Iran yafanyia majaribio kwa mafanikio kombora lake jipya kutoka katika nyambizi
(last modified Sun, 24 Feb 2019 07:57:29 GMT )
Feb 24, 2019 07:57 UTC
  • Iran yafanyia majaribio kwa mafanikio kombora lake jipya kutoka katika nyambizi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanyia majaribio kwa mafanikio kombora lake jipya la majini kwa ardhi kwa kutumia nyambizi yake aina ya Ghadir.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, msemaji wa Mazoezi ya Kijeshi ya Velayat 97, Admeri Hamze Ali Kaviani amesema leo kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa Iran kufanya majaribio kama hayo kutoka kwenye kina kirefu ya maji na kupiga kwa mafanikio shabaha iliyokusudiwa hasa kutokana na vizuizi na hatari mbalimbali zilizopo kwenye mashambulizi kama hiyo kama vile kugunduliwa sehemu ilipo nyambizi.

Amesema, kwa ubunifu wa wanasayansi na wataalamu vijana wa Kiirani, majaribio hayo yamefanyika kwa mafanikio na kuzuia hatari na vizuizi vyote vya kijeshi vinavyoambatana na suala hilo.

Moja ya mokombora ya Jeshi la Majini la Iran

 

Msemaji huyo wa luteka ya kijeshi ya Velayat 97 amesema pia kwamba nyambizi nyingine za jeshi la majini la Iran kama vile nyambizi nzito aina ya Tareq na Fateh nazo zina uwezo wa kufanya mashambulizi kama hayo na kutojulikana zimefanyia wapi.

Mwanzoni mwa mazoezi hayo ya majini ya kijeshi, Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran, Admiral Hossein Khanzadi alisema kuwa, katika mazoezi hayo, jeshi hilo litafanyia majaribio makombora ya Cruise ya baharini na makombora ya torpedo na mengine ya kulenga manuwari za kivita na nyambizi za chini ya maji.

Mazoezi hayo makubwa ya kijeshi ya Velayat 97 yanafanyika miezi kadhaa baada ya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) kufanya manuva makubwa ya kijeshi ya aina yake yaliyopewa jina la "Mtume Mtukufu Muhammad SAW 12" karibu na kisiwa cha Qeshm kilichoko Ghuba ya Uajemi.

 

Tags