Iran kutuma misaada Venezuela
(last modified Mon, 25 Feb 2019 04:20:09 GMT )
Feb 25, 2019 04:20 UTC
  • Iran kutuma misaada Venezuela

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutuma msaada wa dawa na vifaa vya kitiba Venezuela, nchi ambayo imekuwa ikikabiliwa na njama za mababeru wakiongozwa na Marekani ambao wanataka kuipindua serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran Mahdi Pirsalehi amesema mbali na kutuma dawa na vifaa vya kitiba Venezuela, Iran pia iko tayari kuipa nchi hiyo uwezo wa kitiba kwa mujibu wa mapatano baina ya pande mbili yaliyotiwa saini mwaka 2018.

Ametoa kauli hiyo alipokutana na Ruben Dario Molina Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela mjini Tehran Jumapili.

Mapema Jumapili pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alikutana na  Dario Molina ambapo walijadili matukio ya hivi karibuni katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Wawili hao walilaani vikali sera za Marekani za kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine. Katika mkutano huo Dario Molina alimfahamisha Zarif kuhusu hali ya hivi sasa ya kisiasa katika nchi yake huku akiipongeza Iran kwa kusaidia kuboresha hali ya Venezeula.

Rais Maduro wa Venezuela

Kwa uapnde wake Zarif alipinga uingiliaji wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya Venezuela na kubainisha kuwa Iran itaendelea kuunga mkono serikali na taifa la Venezuela. Aidha amesema Iran inaunga mkono pendekezo la mazungumzo ya kisiasa baina ya serikali na wapinzani ili kutatua tafauti zao.

Itakumbukwa kuwa, Rais Nicolas Maduro alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika kidemokrasia mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela na kuidhinishwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 6.

Hata hivyo, tarehe 23 mwezi uliopita wa Januari 2019, na kwa baraka kamili za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na baadhi ya nchi za eneo la Amerika ya Latini, Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela alijitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo suala ambalo ni kinyume kabisa na katiba ya nchi hiyo.

Nchi nyingi duniani ikiwemo Iran, Russia, China, Cuba, Uturuki, Afrika Kusini, Uruguay n.k, zinapinga vikali kitendo hicho kilicho kinyume na katiba ya Venezuela na uingiliaji wa madola ya kibeberu hasa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

 

Tags