Pezeshkian: Mandela atakumbukwa kwa mapambano yake dhidi ya dhulma
(last modified Thu, 24 Oct 2024 07:19:35 GMT )
Oct 24, 2024 07:19 UTC
  • Pezeshkian: Mandela atakumbukwa kwa mapambano yake dhidi ya dhulma

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amemuenzi na kumpongeza kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela kutokana na jitihada na mapambano yake dhidi ya dhulma na ukandamizaji.

Katika mkutano na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, pambizoni mwa mkutano wa 16 wa viongozi wa kundi la BRICS unaofanyika huko Kazan nchini Russia, Rais Pezeshkian ameeleza kuwa, jina la Afrika Kusini duniani linafungamana na Nelson Mandela na mapambano dhidi ya dhulma na ukandamizaji.

Dakta Pezeshkian ametaja mitazamo ya kupigania haki na uadilifu ya Pretoria katika masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Israel kutokana na jinai za kivita za utawala huo haramu dhidi ya Gaza, kuwa ni zao la mtazamo wa kupigania usawa wa hayati Mandela.

Rais wa Iran amesema, "Leo tunashuhudia dhana potofu ya haki za binadamu duniani na kutokea kwa uhalifu kwa jina la haki za binadamu. Kuongezeka kwa ushawishi wa BRICS na kuimarisha maingiliano kati ya wanachama wake kunaweza kurekebisha hali ya sasa isiyo ya haki."

Bendera za nchi wanachama wa BRICS

Rais wa Afrika Kusini kwa upande wake amesema kuwa, uanachama wa Iran katika BRICS utaimarisha umoja wa jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, nchi wanachama zinataka maendeleo ya pamoja na sio maendeleo ya upande mmoja ambayo yanatoa muhanga maslahi ya wengine.

Ramaphosa amebainisha kuwa, wananchi wa Palestina wanapaswa kujiamulia mustakabali wao wenyewe na kusisitiza kwamba, Afrika Kusini daima imekuwa ikiunga mkono uhuru na haki za watu wa Palestina.

Tags