JCPOA ya staili ya Ulaya ya kumridhisha na kumhudumia Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52618-jcpoa_ya_staili_ya_ulaya_ya_kumridhisha_na_kumhudumia_trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, madai ya nchi tatu zinazounda Troika ya Ulaya dhidi ya mpango wa makombora wa Iran ni aina mojawapo ya kukwamisha mambo na kufanya yale yanayoipendeza na kuiridhisha Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 04, 2019 07:51 UTC
  • JCPOA ya staili ya Ulaya ya kumridhisha na kumhudumia Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, madai ya nchi tatu zinazounda Troika ya Ulaya dhidi ya mpango wa makombora wa Iran ni aina mojawapo ya kukwamisha mambo na kufanya yale yanayoipendeza na kuiridhisha Marekani.

Mohammad Javad Zarif ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: Baada ya kupita mwaka mmoja tangu Marekani ijitoe kinyume cha sheria katika JCPOA, Ulaya haina uwezo wa kuonyesha irada yake ya kisiasa kwa kutoa changamoto ya kukabiliana na ugaidi wa kiuchumi wa Marekani; na haina uwezo pia hata wa kuanzisha njia ya kibenki kwa ajili ya misaada ya kibinadamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: Katika mazingira kama haya, nchi tatu za Ulaya zinaushinikiza Umoja wa Mataifa kuhusiana na uwezo wa ulinzi wa Iran ili kumridhisha rais wa Marekani, Donald Trump.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif

Mabalozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumanne walidai katika barua waliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwamba ustawishaji teknolojia ya makombora, hatua ya Iran ya kurusha roketi la kubebea satalaiti na kuzindua makombora mawili mapya ya balestiki ni hatua zinazopingana na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Madai hayo ya mara kwa mara ya nchi tatu za Ulaya kuhusu uwezo wa makombora wa Iran yametolewa na nchi hizo kwa lengo la kukwepa masuulia ziliyonayo ya kutekeleza ahadi na majukumu yao katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ikiwemo kuhakikisha zinaendeleza ushirikiano wa kiuchumi na Iran.

Baada ya Marekani kujitoa kwenye JCPOA, nchi za Ulaya, ambazo zilikuwa zikisisitiza kwamba, zitaendelea kutekeleza makubaliano hayo na kujitahidi kuhakikisha Iran inanufaika na faida zake za kiuchumi, hivi sasa si tu hazioneshi kuwa na irada wala azma yoyote ya kweli, lakini pia zinafanya uafriti wa kukwamisha suala hilo.

Awali Umoja wa Ulaya uliahidi kulinda na kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika JCPOA

Utoaji visingizio unaofanywa na nchi za Ulaya na kukariri madai ambayo hayana uhusiano wowote na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kunaonyesha kuwa, Ulaya si ya kuaminika na vile vile haina uwezo wa kufanya lolote bila ridhaa ya Marekani.

Kushindwa nchi za Ulaya kutekeleza utaratibu na mfumo wa fedha kwa ajili ya kuendeleza mawasiliano ya kifedha na kiuchumi na Iran na wakati huo huo kuzusha madai kwamba Iran inakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama, ni upigaji hatua unaofanywa na nchi hizo wa kufuata njia ile ile aliyoianisha Trump baada ya kujitoa kwenye JCPOA.

Rais wa Marekani alitumia kisingizio hicho kwa kudai kwamba, JCPOA si makubaliano yaliyokamilika kwa sababu hayajajumuisha mpango wa makombora na ushawishi wa kieneo wa Iran; na kwa sababu hiyo akajitoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia.

Msimamo wa sasa wa nchi tatu za Ulaya na hatua yao ya kuushinikiza Umoja wa Mataifa uchunguze mpango wa makombora wa Iran, ni ishara nyingine ya jinsi nchi za Ulaya zinavyofuata mdundo wa ngoma inayopigwa na Trump na kwa mara nyingine kuwathibitikia watu wote kwamba Ulaya haina uwezo wa kujichukulia maamuzi kwa uhuru.

Kudai nchi tatu za Ulaya kwamba mpango wa makombora wa Iran, wa anga za mbali pamoja na majaribio yake ya makombora yanakiuka azimio nambari 2231 ni ithbati ya undumakuwili zilionao nchi hizo wenye lengo pia la kufifisha udhaifu wao wa kushindwa kukabiliana na Marekani.

Kuhusiana na suala hilo, balozi na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa jibu kwa madai ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kwamba Iran imekiuka azimio nambari 2231, kwa kuzitaka nchi za Ulaya ziachane na utumiaji huo wa vigezo vya kiundumakuwili; na badala yake vishughulikie matatizo halisi na ya msingi kama kujitoa Marekani katika JCPOA pamoja na mwenendo haribifu na silaha za mauaji ya halaiki ya Israel. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, naye pia amebainisha mara kadhaa kuwa, kitu pekee ambacho azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka Iran ni kutounda makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia na akasisitiza kwamba, Iran haina mpango wa nyuklia wa masuala ya kijeshi.

Kuimarisha uwezo wa kiulinzi na wa makombora na kuwa na ushawishi athirifu kieneo kunafanyika kwa ajili ya kuzingatia manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na hakuna nchi yoyote inayokubali kuipatia nchi nyingine mamlaka ya kuiamulia kuhusu mambo hayo mawili muhimu yanayodhamini nguvu na uwezo wake.

Katika hali kama hii, kitendo cha nchi za Ulaya kumhudumia na kumfurahisha Trump kwa kuushinikiza Umoja wa Mataifa, hakitaweza katu kuiburuza Iran na kuifikisha kwenye hali iliyozitinga nchi za Ulaya hivi sasa kutokana na udhaifu wao na kushindwa kwao kuwa na irada huru na ya kujitegemea.

Iran itaendelea kuimarisha mambo yanayoifanya iwe na nguvu, bila kujali makelele na mashinikizo ya kisiasa ya Magharibi, na wala haitafanya mazungumzo na yeyote juu ya suala hilo. Ni kama alivyosisitiza mara kadhaa Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran, Meja Jenerali Mohammad Bagheri ya kwamba: Uwezo wa kiulinzi wa Iran ukiwemo wa nguvu za makombora, hauwezi katu kujadiliwa kwa namna yoyote ile.../