Sakata la usalama, Waziri wa Ulinzi wa Nigeria ajiuzulu
-
Waziri wa Ulinzi wa Nigeria ajiuzulu kufuatia sakata la ukosefu wa usalama
Waziri wa Ulinzi wa Nigeria, Mohammed Badaru Abubakar amejiuzulu, katika kipindi ambacho nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa usalama unaojumuisha utekaji nyara wa watoto wa shule kwa wingi.
Kuondoka kwake kunakuja baada ya Rais Bola Tinubu kutangaza "hali ya dharura ya usalama wa taifa” wiki iliyopita, huku nchi ikihangaika kukabiliana na wimbi la utekaji nyara wa watu wengi, ambapo mamia ya watu, hasa watoto wa shule, walitekwa ndani ya siku chache mwezi uliopita.
Msemaji wa Tinubu, Bayo Onanuga, alisema katika taarifa kwamba Abubakar, mwenye umri wa miaka 63, anaacha wadhifa huo mara moja kwa sababu za kiafya.
Rais Tinubu anakabiliwa na mashinikizo baada ya karibu watu 400, zaidi ya 300 kati yao wakiwa wanafunzi, kutekwa nyara katika moja ya wimbi kubwa zaidi la utekaji nyara nchini humo katika siku za hivi karibuni.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na utekaji nyara huo na mamlaka husika huko Nigeria zimesema vikosi vya kimkakati vimetumwa pamoja na wawindaji wa eneo hilo kuwaokoa watoto hao.
Juhudi za utafutaji na uokoaji zinaendelea ili kuokoa wanafunzi waliosalia huku wazazi wao wakihangaika huku na kule katika hali ya mfadhaiko na kukata tamaa.
Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Nigeria kwa madai ya mauaji ya Wakristo. Serikali ya Nigeria imepinga madai hayo, ikiyataja kuwa ni taswira potofu ya hali halisi. Serikali ya Nigeria inasema raia wote wa nchi hiyo, wawe Wakristo au Waislamu ni waathirika wa mashambulizi ya magaidi na watekaji nyara.