Apr 08, 2019 07:58 UTC
  • Larijani: Nchi za Kiislamu zimeitelekeza Palestina

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Ali Larijani ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya nchi za Kiislamu ya kuitelekeza na kuiweka pembeni kadhia muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, ambayo ni Palestina.

Dakta Larijani aliyasema hayo jana Jumapili katika mji mkuu wa Qatar, Doha, katika mazungumzo yake na mwenzake wa Oman Sheikh Khaled Bin Hilal Al-Maouli, pambizoni mwa mkutano wa 140 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU).

Amesisitiza kuwa, Quds ni mji mkuu wa kudumu wa Palestina na kwamba hatua yoyote iliyo kinyume na hivyo ni kukanyaga maamuzi ya Umoja wa Mataifa na haikubaliki.

Kadhalika Spika wa Bunge la Iran amekutana na kufanya mazungumzo na mwenza wa Jordan, Atef Tarawneh, ambapo amebainisha kuwa, mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel yataendelea na kwamba  kukandamizwa muqawama wa Wapalestina hakutazuia kufikiwa malengo ya raia hao.

Dakta Larijani na Atef Tarawneh

Waraka wa kutangazwa uhuru wa Palestina ambao ulisainiwa katika duru ya 19 ya vikao vya dharura vya Baraza la Taifa la Palestina huko Algeria mwaka 1988, umezipelekea nchi 138 duniani kuitambua Palestina kufikia sasa.

Kadhalika Spika wa Bunge la Iran na wenzake wa Qatar na Jordan wamesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati Tehran na Muscat na Tehran na Amman, hususan katika uga wa biashara na uchumi.

Tags