Kiongozi: Walanguzi na wahalifu katika mitandao ya kijamii washughulikiwe vikali
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema jeshi la polisi lina nafasi muhimu katika kulinda usalama katika Intaneti na mitandao ya kijamii na kuongeza kuwa: "Jeshi la polisi linapaswa kukabiliana vikali na walanguzi wa bidhaa na wahalifu wa intaneti na mitandao ya kijamii."
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumapili hapa mjini Tehran alipokutana na makamanda na maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Akiashiria suala la 'kudumisha usalama katika intaneti na mitandao ya kijamii' amesema: "Intaneti na mitandao ya kijamii leo inatumika kwa mapana katika maisha ya wananchi na pamoja na kuwa ina manufaa na suhula pia ina hatari kubwa."
Kiongozi Muadhamu amesema kukosekana usalama katika Intaneti na mitandao ya kijamii ni jambo ambalo linawasababishia wananchi hasara na kwa hiyo ni jukumu la Jeshi la Polisi kudumisha usalama katika intaneti na mitandao ya kijamii.
Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa, sharti la kupatikana ustawi wa kiuchumi ni kuwepo usalama na kuongeza kuwa: "Moja ya vizingiti katika kufikia ustawi wa uzalishaji ni ulanguzi wa bidhaa ambapo tatizo hilo leo linaonekana katika pande zote yaani mbali na ulangauzi wa bidhaa kutoka nje leo pia bidhaa ambazo wananchi wanazihitaji za sekta ya kilimo zinapelekwa nje ya nchi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa,'kuzuia ununuzi na uuzaji wa silaha ni moja ya majukumu mengine ya Jeshi la Polisi nchini Iran na kuongeza kuwa: "Katika baadhi ya nchi kama vile Marekani, biashara ya silaha ni huru kutokana na maslahi ya mafia katika mashirika ya utegenezaji sialaha na jambo hilo limewasababishia wananchi tatizo." Ameongeza kuwa, nchini Iran hakuna tatizo kama hilo kwani uuzaji na ununuzi wa silaha ni kinyume cha sheria na hali hiyo inapaswa kuendelea.
Kiongozi Muadhamu amesisitza kuhusu ulazima wa kuzuia uuzaji na ununuzi wa silaha katika mitandao ya kijamii na kuongeza kuwa: "Muuaji wa mwanazuoni wa kidini mjini Hamedan alisambaza taswira katika Instagram yenye aina nne ya silaha zake na hivyo ni jukumu la Jeshi la Polisi kukabiliana na uovu kama huo.
Ayatullah Khamenei aidha amesema, 'nguvu', na 'ukarimu' wa Jeshi la Polisi ni nukta mbili ambazo zinakamilishana na huku akiashiria jitihada za usiku na mchana za maafisa wa Jeshi la Polisi hasa katika siku za likizo amesema katika kadhia ya mafuriko hivi karibuni, Jeshi la Polisi limetoa huduma nzuri kwa wananchi walioathiriwa.