Uchaguzi na umoja wa kitaifa nchini Iran
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio makala yetu ya wiki ambayo itaangazia uchaguzi na umoja wa kitaifa nchini Iran.
Uchaguzi ni mojawapo ya matukio muhimu ya kisiasa ambayo yana majukumu maalumu na muhimu. Mojawapo ya majukumu hayo ni taathira zake muhimu katika umoja wa kitaifa kama msingi wa maisha, uwezo na maendeleo endelevu katika jamii. Taathira hizo pia zinaweza kuwa chanya au hasi. Moja ya sababu zinazowafanya maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatilia chaguzi zinazofanyika nchini Iran na kujaribu kuzuia ushiriki mkubwa wa wananchi katika chaguzi hizo, kwa kutumia mikakati na propaganda zao kubwa inahusiana na jukumu hili la kuliunganisha taifa. Kama alivyobainisha Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kushiriki kwa wingi wananchi katika medani ya uchaguzi ni dhihirisho la umoja wa kitaifa. Ayatullah Khamenei anasema, uchaguzi ni sababu ya kuwepo umoja wa kitaifa, na umoja wa kitaifa ni nguzo ya usalama wa kitaifa, na usalama wa kitaifa unaifanya nchi kuwa na nguvu na imara.
Katika Aya ya 103 ya Suratu Al-Imran, Qur’ani Tukufu inataja migawanyiko, hitilafu na mifarakano kuwa ni ncha ya shimo la moto wa vita, na kwamba umoja na mshikamano huondoa hatari ya kutumbukia kwenye shimo hilo. Vilevile Mtume Muhammad (saw) anasema: Msikhitalifiane, kwani waliokuwa kabla yenu walihitalifiana, wakaangamia.
*********
Swali linalojitokeza hapa ni kuwa, uchaguzi unasababisha vipi umoja wa kitaifa? Katika kujibu swali hili tunaweza kusema kuwa, kimsingi ushiriki wa jamii una taathira kubwa na unaandaa mazingira ya utangamano na mshikamano wa kitaifa katika jamii. Kufanyika uchaguzi kunaandaa uwanja mzuri wa kushirikishwa wananchi katika nyanja zote za jamii katika mchakato wa kitaifa; na kwa hakika suala hili ndilo linaloufanya uchaguzi kuwa mhimili wa umoja na mshikamano wa kitaifa ambavyo pia huimarisha nchi na kuipa uwezo mkubwa zaidi. Katika uwanja huo, tusisahau kuwa, wakati wa vita vya kujihami kutakatifu maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walishindwa kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya zana zote za kisasa walizokuwanazo na kuungwa mkono kwa pande zote na nchi mbalimbali. Hii ni kwa sababu mshikamamo wa kitaifa nchini Iran ulikuwa wa kiwango cha juu sana; na wananchi walishirikiana bega kwa bega na wanajeshi vitani dhidi ya adui wa taifa.
Ushiriki mkubwa na wa hamasa wa wananchi kwenye uchaguzi ni sawa na wananchi kuunga mkono utambulisho wa kitaifa na wa serikali yao ya kitaifa. Kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi kuna maana ya kusisitiza utambulisho wao wa kitaifa. Kwa sababu hiyo, moja ya matokeo muhimu ya ushiriki mkubwa wa wananchi katika masuala ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa wingi katika uchaguzi ni kustawisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Taifa linaweza kupata "umoja wa kitaifa" kupitia umoja na mshikamano wa ndani, na kuupanua zaidi katika matabaka mbalimbali ya kijamii. Moja ya maeneo ambako umoja huu unaundika ni katika uchaguzi. Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kuhusiana na suala hili kwamba: "Umoja wa kitaifa ni kati ya mambo yanayoifanya nchi kuwa imara na na yenye nguvu. Ni wazi kuwa umoja wa kitaifa ni kizuizi na ukuta imara ulioinuliwa mbele ya adui. Umoja wa kitaifa ulikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Mapinduzi kiislamu na kisha katika maendeleo ya mapinduzi hayo."
Suala jingine muhimu ni kuwa, ushiriki wa kisiasa katika uchaguzi ni sawa na uungaji mkono wa wananchi kwa serikali ya kitaifa. Serikali ya kitaifa ni mojawapo ya mambo ambayo ni a mageni kwa eneo la Asia Magharibi, kwa sababu suala la umoja wa kitaifa halijaasisiwa vyema katika aghalabu ya nchi za eneo hili. Hii ni katika hali ambayo, taifa na utaifa nchini Iran ni suala halisi la uhakika ambalo lina mizizi ya kihistoria. Inaonekana kuwa stratejia kuu ya maadui mkabala wa wananchi wa Iran, ni kudhoofisha utambulisho wa kitaifa. Aidha lengo kuu la statejia hiyo ni kudhoofisha serikali ya kitaifa katika Iran ya leo. Moja ya baraka za mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi la uchaguzi ni kudhihirisha uungaji mkono wa wananchi kwa mfumo tawala. Bila shaka ushiriki wa wananchi wa Iran katika uchaguzi una taathira ya kipekee kwa mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na mamlaka ya nchi hii katika eneo na duniani kwa ujumla. Hakuna kitu chenye nguvu zaidi kwa nchi kuliko ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya kitaifa. Japokuwa nguvu za kijeshi, kisiasa na kiuchumi zina nguvu na zinaiwezesha nchi, lakini hakuna hata kimoja kinacholingana na ushiriki na mahudhurio ya watu. Wananchi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa na mahudhurio ya hamasa kubwa katika chaguzi zote zilizopita kwa sababu wanajua kuwa kuwepo kwao kunaimarisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa maana halisi ya neno hilo.
Katika upande mwingine ni kuwa, kama ambavyo ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi ni sawa na kuunga mkono waziwazi serikali ya kitaifa; vivyo hivyo ukosefu wa uungaji mkono wa wananchi kwa serikali ya kitaifa uhudumia malengo ya maadui wa mfumo tawala. Ayatullah Khamenei Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema: "Umoja wa kitaifa ndio kitu kinachoweza kuunga mkono juhudi zote za viongozi wa serikali, wanamapambano na watetezi wa nchi na Mapinduzi ya Kiislamu". Bila ya Umoja wa kitaifa, nchi hii haitakuwa na nguvu yake kubwa na nguzo ya maendeleo."
Taifa kubwa la Iran pia linafahamu vyema kwamba athari za uchaguzi kwa umoja wa kitaifa zinaweza kuwa mbaya pale ushiriki wa wananchi katika uchaguzi unapokuwa mdogo. Ni dhahir shahir kuwa kadiri ushiriki mkubwa wa wananchi unavyoweza kuimarisha kiwango cha umoja wa kitaifa, ndivyo ushiriki mdogo na wa kiwango cha chini pia unavyoweza kutuma ujumbe kwamba umoja wa kitaifa umedhoofika. Wakati huo huo, ushiriki dhaifu unaweza kutuma ujumbe kuwa kuna pengo na mwanya kati ya wananchi na serikali. Ndio maana maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran wametoa zingatio mahsusi kwa suala la uchaguzi. Hivi sasa ambapo kuna matatizo ya kiuchumi hasa kutokana na vikwazo vya kidhulma dhidi ya nchi hii; maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameelekeza macho yao kwenye masanduku ya kupigia kura katika fremu ya vita vya kipropaganda na hivyo kutumia suala hili kama jukwaa jingine la makabilianao kati yao na Jamhuri ya Kiislamu. Madui hao wanafuatilia suala la kuwaweka mbali wananchi na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia masanduku ya kura; na wanafanya kila wawezalo kudhoofisha utambulisho na umoja wa kitaifa wa Iran kwa kuvuruga ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.
Duru ya 12 ya uchaguzi wa Majlisi ya ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) na duru ya sita ya uchaguzi wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran zimepangwa kufanyika tarehe 11 mwezi Esfand 1402 Hijria shamsia sawa na Machi Mosi mwaka 2024; ambapo hivi sasa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanakodolea macho chaguzi hizo na masanduku ya kura kuliko wakati mwingine wowote. Mara hii maadui wameulenga umoja wa kitaifa wa Iran na Wairani katika hujuma zao, na wanajaribu kuwachochea wananchi wasishiriki bali wasusia uchaguzi huo.
Katika miaka ya hivi karibuni, sera kuu na muhimu zaidi ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa kuzusha migogoro ya ndani na kuibua pengo kati ya wananchi na serikali. Lengo muhimu zaidi la Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo vipya kuanzia mwaka 2018 na kuendelea, lilikuwa kuwawekea mashinikizo wananchi katika masuala ya kimaisha na kugeuza hali ya kutoridhika wananchi kuwa mgogoro wa kiusalama na hatimaye kuanzisha machafuko dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Ghasia na machafuko ya mwaka jana nchini Iran ni miongoni mwa matukio ambayo yaliungwa mkono na kufadhiliwa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ambao walifanya juu chini kuyaendeleza kwa miezi kadhaa. Hivi sasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mbioni kufanya uchaguzi wa 12 wa Bunge na wa 6 wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ambazo ni chaguzi za 40 na 41 katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, tunashuhudia muendelezo wa sera za maadui ma prppaganda zao chafu za kkuwataka wananchi wasishiriki kwa wingi katika zoezi hilo la kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua wawakilishi wao.
Hata hivyo njama hii, kama zilivyokuwa za miaka iliyopita, itafeli na kugonga mwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na nguvu na irada ya wananchi shupavu wa Iran ya Kiislamu.