Ayatullah Khamenei: Marekani haiwezi kufanya chochote kuhusu mradi wetu wa nyuklia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema urutubishaji wa urani ndio ufunguo wa suala la nyuklia la Iran, akipuuzilia mbali pendekezo la Marekani kwa Tehran la kusimamisha kikamilifu urutubishaji wa madini hayo (ya urani).
Kiongozi Muadhamu amesema, "Neno la kwanza la Marekani ni kwamba Iran haipaswi kuwa na teknolojia ya nyuklia. Majibu yetu kwa madai hayo ya kipuuzi ya Marekani yako wazi: Hawawezi (kuthubutu) kufanya kosa lolote katika hili."
Amesisitiza kuwa, teknolojia ya nyuklia ni sekta ya msingi ambayo nchi zote zina haki ya kuitumia kwa amani. Amesema teknolojia hiyo inaleta uhuru kwa mataifa katika sekta ya nishati pamoja na maeneo mengine, yakiwemo dawa na tiba. Amebainisha kuwa, "bila urutubishaji (wa urani), teknolojia ya nyuklia kimsingi haina maana."
Kiongozi Muadhamu amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yenye mfumo wa kisiasa unaostawi, imara na wenye mamlaka uliotokana na mapinduzi makubwa, yameushangaza ulimwengu wa Magharibi. Amesema licha ya kufariki dunia Imam Rouhullah miaka 36 iliyopita, lakini Mfumo wa kisiasa wa Iran tangu wakati huo umeendelea kuimarika kwa uthabiti na nguvu.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumatano alipokuwa akihutubia katika hafla ya kuadhimisha miaka 36 ya kufariki dunia Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Hayati Imam Khomeini (MA) na kueleza kuwa, "Athari za Mapinduzi ya Kiislamu ya Imam Khomeini zinaonekana machoni pa watu duniani kote."

"Kuporomoka kwa kasi kwa nafasi ya Marekani duniani kunaathiriwa na uwepo wake, na chuki dhidi ya Wazayuni inaathiriwa na mapinduzi yake," Ayatullah Khamenei amesema.
"Hawakuamini kwamba Mapinduzi haya na Imam (Khomeini) wangeweza kuwafutilia mbali Wamarekani na Wazayuni, ambao walikuwa wametawala kila kitu nchini Iran kwa miaka mingi, na wangeweza kuwafukuza nchini."
Imam Khamenei amegusia aina zote za njama dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambazo amesema, hazina mfano katika mapinduzi yoyote yanayojulikana duniani. Amesema Jamhuri ya Kiislamu imestahimili njama, mipango na uadui wote.

Kiongozi Muadham ameeleza kuwa, uhuru wa kitaifa haumaanishi kutengwa na kukosa uhusiano na ulimwengu; ina maana ya taifa la Iran kusimama kidete lenyewe.
"Uhuru wa kitaifa unamaanisha kuwa nchi haipaswi kusubiri taa ya kijani (kibali) au nyekundu (zuio) kutoka kwa Marekani na washirika wake; kipengele muhimu cha uhuru wa kitaifa ni kanuni ya 'tunaweza'," Ayatullah Khamenei ameongeza.