Oct 01, 2024 11:20 UTC
  • Sayyid wa Muqawama, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Karibuni kuwa nami katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.

Unakaribia kutimia mwaka mmoja wa kumbukumbuku ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa Oktoba 7, 2023. Operesheni hiyo ilitokea baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi na upelelezi uliofanywa na Hamas, uliobaini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unajiandaa kufanya shambulio kubwa la pande zote dhidi ya Ghaza.

Kwa kulibaini hilo- na kwa sababu ya jinai za kinyama zilizowaandama wananchi madhulumu wa Palestina kwa takribani miaka 75 sasa, mbali na mzingiro wa kiuchumi na wa kuzuia kuingizwa dawa katika Ukanda wa Ghaza kwa muda wa miongo miwili, na hivyo kuwaweka watu wa Ghaza kwenye dhiki, tabu na mateso makubwa- harakati ya Muqawama ya Hamas iliamua kushambulia maeneo ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni ili kwanza, kutoa mjibizo kwa jinai za mtawalia za Israel za kuwaua kila uchao Wapalestina; na pili kupunguza athari za shambulio kubwa lililokuwa limeandaliwa kufanywa na utawala huo wa Kizayuni na kuianika hadharani njama hiyo chafu. Kwa mtazamo wa Hamas, na kwa mujibu wa taarifa yake iliyokuja kutoa siku chache baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, operesheni hiyo ilikuwa hatua ya lazima kuchukuliwa na jibu la kutarajiwa kwa ajili ya kukabiliana na mipango na njama zilizokuwa zimeandaliwa kwa lengo la kulifuta moja kwa moja suala la Palestina. Operesheni hiyo ilitekelezwa pia ili kukabiliana na mipango ya utawala wa Israel ya kuihodhi ardhi ya Palestina, Kuiyahudisha na kuudhibiti Msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.

Katika sehemu moja ya taarifa yake hiyo ya kurasa 18 iliyoandaliwa kwa anuani: "Hii ndiyo simulizi yetu sisi…ni kwa nini Operesheni ya Al-Aqsa?", Hamas imesema: "ni kwa miaka na miaka, wananchi wetu wameteseka kwa anuai za dhulma, uonevu, kuporwa haki zao za msingi na kuandamwa na sera za ubaguzi wa Apathaidi; na kwa zaidi ya miaka 17, Ukanda wa Ghaza umekabwa na mzingiro kandamizi, kiasi cha kuugeuza kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani… "Kimbunga cha Al-Aqsa" kilikuwa na ulazima ili kukomesha mzingiro huu wa kidhalimu dhidi ya Ghaza na ni hatua ya kutarajiwa ili kujikomboa na uvamizi. Operesheni ya Muqawama ilikuwa pia hatua ya kutarajiwa, kwa ajili ya Wapalestina kujitawala na kuwa huru kama yalivyo mataifa mengine duniani, na kuwa na haki ya kujiamulia majaaliwa yao".

Vyombo vya habari vya Israel viliielezea operesheni hiyo kuwa ni ya aina yake katika historia na kipigo kikubwa ambacho haujawahi kukishuhudia utawala huo. Wapalestina wa Ghaza na kambi ya Muqawama ambao wamekuwa wakiamini kwamba kufa shahidi kwa heshima ni bora kuliko kumpigia magoti adui na kusalimu amri, hadi leo hii wamesimama imara kuzikabili hatua zote za kinyama za jeshi katili la Kizayuni dhidi ya operesheni ya Hamas na kutoa mhanga Mashahidi wengi sana.

Sambamba na hayo, ni nchi chache na watu wachache pia waliojitokeza kuiunga mkono hatua hiyo ya Hamas ya kupigania kujikomboa. Watu hao wamesimama bega kwa bega na Wapalestina madhulumu wa Ghaza, ambao kwa takribani mwaka mmoja sasa, wame miminiwa zaidi ya tani elfu 80 za mabomu na utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu, yaani utawala wa Marekani. Watu wa mwanzo kabisa mashujaa na wenye ghera waliojitokeza kulikabili jeshi la utawala wa Kizayuni kwa ajili ya Wapalestina wa Ghaza walikuwa ni wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon.

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah

Katibu Mkuu wa harakati hiyo, Sayyid Hassan Nasrullah, alisimama kwa uwezo wake wote na kuingia kwenye medani ya mapambano ili kutekeleza kile alichokiita ‘kuushughulisha’ utawala wa Kizayuni kaskazini ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ili kupunguza hilaki ya mabomu na makombora wanayomiminiwa watu wa Ghaza.

Katika mjibizo iliotoa kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kupitia mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Ghaza, Hizbullah ya Lebanon ilianzisha mashambulio dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni na ikatangaza kuwa, uungaji mkono wake kwa Wapalestina hautasitishwa mpaka vitakapokomeshwa vita vya Ghaza na mauaji ya Wapalestina. Hii ni ahadi aliyojifunga nayo kikamilifu Katibu Mkuu wa harakati hiyo ya Muqawama. Ni Sayyid Hassan Nasrullah, ambaye alikuwa akisisitiza kwa kusema: “Ikiwa tutabaki hai ni washindi, na kama tutakufa shahidi tutakuwa washindi pia”.

Katika muda huu unaokaribia mwaka mmoja ulioanza Oktoba 7, shakhsia muhimu kadhaa wa kuanzia Ghaza, Syria, Lebanon, Iraq na Iran wameuliwa shahidi na utawala wa kinyama wa Kizayuni. Ni shakhsia wakubwa, ambao wamefanya kila waliloweza kuwatetea wanaodhulumiwa; nasi sote tunajua kama kuwatetea wanaodhulumiwa na kukabiliana na dhulma kuna gharama zake, ambazo humgharimu kila mtetezi wa uhuru na haki; na hilo analijua vyema kila anayejitosa kwenye medani hiyo.

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah

Katika kuendeleza mauaji yake ya kikatili, magharibi ya Ijumaa ya tarehe 27 Septemba, jeshi la utawala wa Kizayuni lilifanya shambulio la kinyama na ambalo halijawahi kushuhudiwa katika eneo la makazi ya raia la Adh-Dhaahiya Kusini, kwenye viunga vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Lengo la shambulio hilo lilitajwa kuwa ni kuangamiza makao makuu ya kamandi ya Hizbullah; na kwa hiyo ndege za kivita za utawala wa Kizayuni aina ya F15 zilishambulia vikali na mtawalia eneo hilo kwa mabomu ya kubomolea mahandaki yenye uzito wa paundi elfu mbili. Asubuhi ya Septemba 28 jeshi la utawala haramu wa Israel likatangaza kuwa katika shambulio hilo lilimuua shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.

Lakini kabla ya kuendelea zaidi, na tujiulize, Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa nani!

Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa mmoja wa maulamaa wanamapambano na mwanajihadi wa zama hizi wa nchini Lebanon na Katibu Mkuu wa harakati ya nchini humo ya Hizbullah, ambaye kwa miaka kadhaa alisimama imara kukabiliana na jinai za uchokozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni na kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina. Sayyid Hassan, -ambaye kuanzia mwaka 1992, na baada ya kuuliwa shahidi na Wazayuni Katibu Mkuu wa wakati huo wa Hizbullah Sayyid Abbas Musawi alichaguliwa kwa kauli moja na Baraza la Uongozi la harakati hiyo kuwa Katibu Mkuu wake mpya-, katika muda wa zaidi ya miongo mitatu ya kuiongoza Hizbullah, aliweza kuigeuza harakati hiyo kutoka kwenye sura ya taasisi ndogo ya kijeshi, na kuwa jeshi kubwa na imara; na kuitoa kwenye hali ya nguvu ya kitaifa na kuwa nguvu ya kikanda, pamoja na kuwaletea matunda mengi na mafanikio makubwa mno wananchi wa Lebanon na kambi ya Muqawama.

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah katika miaka ya mwanzo ya Ukatibu Mkuu wa Hizbullah

Baadhi tu ya hatua na mafanikio makubwa iliyopata harakati ya Hizbullah chini ya Ukatibu Mkuu wa Sayyid Hassan Nasrullah, ni pamoja na kuzima operesheni ya kijeshi ya Israel ya mwaka 1993 iliyopewa jina la Uwajibikaji na ile ya mwaka 1996 iliyoitwa Zabibu za Ghadhabu; kuulazimisha utawala wa Kizayuni mnamo mwaka 2000 kuondoka kwenye ardhi za Lebanon ulizokuwa umezivamia na kuzikalia kwa mabavu; kulishinda kwa kipigo cha kufedhehesha jeshi la Kizayuni katika Vita vya Siku 33 vya mwaka 2006 na vilevile kuiunga mkono serikali halali ya Syria na kuisaidia katika kuuangamiza ugaidi wa kitakfiri wa kundi la DAESH (ISIS) nchini humo.

Kupata uungaji mkono wa umma wa Walebanoni na kugeuka Hizbullah kuwa vuguvugu la wananchi lililokubalika ndani ya jamii; kujiimarisha harakati hiyo katika uga wa siasa za Lebanon kwa kufika hadi ya kuwa na wawakilishi wengi ndani ya Bunge la nchi hiyo, mbali na wanachama wake kushika nyadhifa za wizara kadhaa serikalini, sambamba na mafanikio ya kijeshi tuliyoyaeleza, yote hayo ni sehemu ya mafanikio ya aina yake aliyopata Sayyid Hassan Nasrullah katika Ulimwengu wa Kiislamu na kumfanya atambulike kama shakhsia muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Waarabu.

Mauaji ya kigaidi ya kumuua shahidi Sayyid Hassan Nasrullah yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni Ijumaa ya Septemba 27, yamefuatiwa na radiamali na mijibizo kadha wa kadha. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa salamu za rambirambi kwa Umma wote wa Kiislamu kwa mnasaba huo; na mbali na kubainisha kwamba, Sayyid Hassan amepata malipo ya miaka na miaka ya Jihadi aliyopigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na tabu alizokabiliana nazo katika kazi hiyo takatifu, amesema: “Sayyid wa Muqawama hakuwa ni shakhsia, bali alikuwa njia na chuo cha fikra; na njia hii itaendelea (kufuatwa). (Kama ambavyo) damu ya Shahidi Abbas Musawi haikupotea, damu ya Shahidi Sayyid Hassan, nayo pia haitapotea”. Aidha amesisitiza kwa kusema: “Msingi alioweka Lebanon na kutoa muelekeo kwa kambi nyingine za Muqawama, sio tu havitatoweka kwa kuondoka kwake, bali vitakuwa madhubuti zaidi kwa baraka za damu yake na za mashahidi wengine wa tukio hili; na kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu, vipigo vitakavyotolewa na kambi ya Muqawama kwa mwili uliochakaa na unaooza wa utawala wa Kizayuni vitakuwa vikali zaidi”.

Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah (kulia) alipomtembelea Kiongozi wa Mapinduzi Ayatullah Khamenei

Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marjaa-Taqlidi mkubwa wa Waislamu wa Kishia wa nchini Iraq amemtaja Sayyid Hassan Nasrullah kuwa ni kiongozi wa kupigiwa mfano na nadra kushuhudiwa katika miongo ya karibuni, ambaye kwa uwezo wake wote aliwasaidia Wairaqi kuikomboa nchi yao kutoka kwenye makucha ya magaidi. Katika salamu zake za rambirambi alizotoa kufuatia kuuawa shahidi Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah, Ayatullah Sistani ameendelea kueleza: “Shahidi huyu mtukufu alitoa mchango mkubwa katika ushindi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na ukombozi wa ardhi za Lebanon; na alichukua misimamo madhubuti ya kuwasaidia wananchi madhulumu wa Palestina, mpaka akaitoa mhanga roho yake yenye thamani kwa ajili ya misimamo hiyo”.

Wanazuoni wengine wakuu wa Kishia ikiwa ni pamoja na Maayatullah Naser Makarim Shirazi, Husain Nuri Hamedani, Jaafar Subhani, Sayyid Musa Shabiri Zanjani, Abdullah Javadi Amoli na Bashir Husain Najafi, nao pia wametoa salamu za rambirambi kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah. Mufti Mkuu wa Oman Sheikh Ahmed bin Hamad Al-Khalili yeye amesema, Sayyid Hassan Nasrullah, alikuwa mwiba kwenye koo ya Wazayuni kwa zaidi ya miongo mitatu, huku akiutolea mwito mrengo wa Muqawama huko Lebanon, Palestina na katika nchi zote za Kiislamu kusimama kidete dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Lakini mbali na maulamaa hao, serikali na viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Iran, Russia, Iraq, Yemen, Cuba na Venezuela pamoja na harakati za Muqawama na ukombozi zikiwemo za Palestina za Hamas, Jihadul-Islami na Fat-h, Ansarullah ya Yemen, A’saaib Ahlul-Haq ya Iraq, Harakati ya Amal ya Lebanon, Sayyid Ammar Hakim, Kiongozi wa Harakati ya Hikma ya Kitaifa ya Iraq, Sayyid Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya Iraq, Chama cha Jamaatul-Islami cha Pakistan na Chama cha Baraza la Maulamaa wa Kiislamu cha Pakistan, wote hao wametoa taarifa za mkono wa pole kwa kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na kulaani shambulio la kigaidi lililofanywa na Israel katika eneo la makazi ya raia nchini Lebanon.

Maandamano ya kumuenzi Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na kulaani mauaji yake

Si vibaya ukaelewa pia kwamba, Iran imetangaza siku tano; nazo Lebanon, Syria, Iraq na Yemen kila moja imetangaza siku tatu za maombolezo kwa mnasaba huo wa kuuawa shahidi Sayyid wa Muqawama, Sayyid Hassan Nasrullah. Sambamba na hayo, wananchi wamefanya maandamano na mijumuiko mbalimbali katika nchi hizo na zingine duniani ikiwemo Pakistan, Kashmir, Jordan, Morocco, Ukingo wa Magharibi Palestina na Bahrain kulaani mauaji ya kigaidi ya Sayyid Hassan Nasrullah na kutangaza uungaji mkono wao kwa Harakati ya Hizbullah. Wasalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags