Mchambuzi wa tiba wa CNN: Mpimeni Trump uzima wa akili
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135712-mchambuzi_wa_tiba_wa_cnn_mpimeni_trump_uzima_wa_akili
Kufuatia vituko alivyofanya hivi karibuni Donald Trump kwa barua aliyomwandikia Waziri Mkuu wa Norway, Dk. Jonathan Reiner tabibu na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha George Washington ametaka rais huyo wa Marekani apimwe uzima wa akili.
(last modified 2026-01-20T23:04:18+00:00 )
Jan 20, 2026 23:04 UTC
  • Mchambuzi wa tiba wa CNN: Mpimeni Trump uzima wa akili

Kufuatia vituko alivyofanya hivi karibuni Donald Trump kwa barua aliyomwandikia Waziri Mkuu wa Norway, Dk. Jonathan Reiner tabibu na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha George Washington ametaka rais huyo wa Marekani apimwe uzima wa akili.

Reiner, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo aliyewahi huko nyuma kuwa tabibu wa makamu wa rais wa zamani wa Marekani Dick Cheney, ameitaja barua hiyo ya Trump kwa Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Storr kuwa ni sababu tosha ya udharura wa kiongozi huyo kupimwa uzima wa akili.

Katika barua hiyo, Trump ameonekana kuunganisha upayukaji wake mkubwa anaofanya kuhusu Marekani kukinyakua kisiwa cha Greenland na suala la yeye kutoshinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka uliopita.

"Barua hii, na ukweli kwamba Rais ametaka barua hiyo zisambaziwe nchi zingine za Ulaya, inapasa ichochee uchunguzi wa pamoja wa vyama vyote viwili katika bunge kuhusu afya ya akili ya Rais," ameandika tabibu huyo katika mtandao wa X.

 

Wito huo umetolewa siku chache tu baada ya Dk. Reiner kumtaka Trump, -ambaye afya yake ya kimwili na uzima wake wa akili vimekuwa vikifuatiliwa kwa karibu zaidi katika miezi ya hivi karibuni-, akafanyiwe vipimo zaidi vya kitiba hususan baada ya kuonekana akisinzia muda wote alipokuwa kwenye hafla nyingine ya kikao.

"Inaonekana rais anapambana na maruweruwe mazito ya usingizi katika wakati wa mchana," ametanabahisha Dk. Reiner.

"Si hali ya kawaida kulala mara kwa mara huku kukiwa na watu kumi na mbili mezani kwako. Inahitaji kutathminiwa", amesisitiza daktari huyo katika andiko lake hilo.../