Mar 09, 2024 12:58 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Hatua ya Meta ya kufuta akaunti za Ayatllah Khamenei ni kinyume cha sheria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani hatua ya kampuni ya Meta ya kuondoa akaunti za Instagram na Facebook za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na kusema ni "kinyume cha sheria na na maadili."

Katika maoni yake yaliyochapishwa kwenye tovuti ya habari yenye makao yake makuu Uingereza ya Middle East Eye, Hossein Amir Abdollahian amelaani "kampuni ya Meta kwa kujaribu kuwadhibiti watetezi mashuhuri wa kadhia ya Palestina.

Amir Abdollahian ameshutumu kusimamishwa "kinyume cha sheria na kinyume cha maadili" kwa akaunti za Ayatullah Khamenei na kusema ni kiashiria cha "kuporomoka kwa maadili na mfumo wa maadili wa ulimwengu."

"Kuzuia akaunti za habari za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu sio tu ni ukiukaji wa uhuru wa kujieleza, bali pia ni dharau kwa mamilioni ya wafuasi wa misimamo na habari zake," amesema Amir Abdollahian.

Siku ya Ijumaa, Meta Platforms, Inc. ilifuta akaunti za Ayatullah Ali Khamenei za lugha ya Kiajemi na Kiingereza.

Hatua hiyo imekuja kufuatia miezi kadhaa ya juhudi za makundi yanayoiunga mkono Israel, ambayo yanajulikana kwa kuwa na ushawishi mkubwa na kuingilia mchakato wa kufanya maamuzi nchini Marekani, mshirika mkubwa wa utawala katili wa Israel.

Kampuni ya Meta inayomiliki mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram, Threads, na WhatsApp, imekuwa ikifuta au kuzuia maudhui za Wapalestina na watetezi wa Palestina kwenye mitandao hiyo tangu Oktoba 7, 2023, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Tags