Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu (1)
Katika kikao chake na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu tarehe 18 Februari mwaka huu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alisema suala la Palestina ni moja ya masuala muhimu zaidi ya ulimwengu wa Kiislamu. Alisema hali ya kusikitisha na kuhuzunisha ya hivi sasa huko Palestina ni matokeo ya kupuuzwa suala hilo na baadhi ya nchi za Kiislamu.
Katika mfululizo wa vipindi hivi, tutazungumzia suala la Palestina, historia yake, nafasi na sababu za umuhimu wake katika ulimwengu wa Kiislamu. “Lau kama nchi za Kiislamu zingesimama kidete na kupambana tangu siku ya kwanza, bila shaka leo hali ya Palestina, eneo la Asia Magharibi na eneo letu ingekuwa tofauti. Leo tungekuwa na nguvu zaidi, umoja zaidi, na hali yetu ingekuwa nzuri zaidi kwa njia tofauti."
Kadhia ya Palestina daima imekuwa miongoni mwa masuala ya kistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika miaka iliyopita, Ayatullah Khamenei daima amekuwa akilichukulia suala la Palestina kuwa suala la kwanza la Umma wa Kiislamu.
Katika kikao chake na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu, katika maadhimisho ya Muba'ath ya Mtume Mtukufu (saw) mwaka huu tarehe 18 Februari, Kiongozi Muadhamu alisisitiza kwa mare nyingine tena kwamba suala la Palestina ni miongoni mwa masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu na kuwa dhulma inayofanyika leo dhidi ya taifa hilo inatokana na udhaifu wa ulimwengu wa Kiislamu na kutokuwepo umoja baina ya nchi za Kiislamu.
Akifafanua kuwa ukandamizaji na dhulma kubwa imekuwa ikifanyika kwa miaka mingi dhidi ya taifa madhulumu la Palestina mbele ya macho ya walimwengu, Kiongozi Muadhamu alikosoa utendaji wa nchi za Kiislamu kuhusiana na suala zima la kuiunga mkono Palestina na kusema pigo dhidi ya taifa hilo ni pigo kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu. Alisema kwa bahati mbaya nchi za Kiislamu zimekaa kimya mbele ya uchokozi huo ambao kwa hakika ni uchokozi dhidi ya nchi hizo zenyewe na dhidi ya Umma wa Kiislamu. Alisema kwa masikitiko kwamba katika baadhi ya matukio, hasa ya hivi karibuni, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikishirikiana na maadui dhidi ya watu wa Palestina. Suala hilo limezifanya nchi za Kiislamu kudhoofika kupita kiasi, kutokuwepo mfungamo unaohitajika baina yazo na hatimaye adui kupata fursa ya kuzidhibiti.
Ayatullah Khamenei alisema kuwa leo madola makubwa ya dunia yanajipa haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiislamu kwa njia moja au nyingine, kwa hoja kuwa zenyewe zimeshindwa kujiendeshea mambo yao, hivyo yanaingilia mambo ya ndani ya nchi hizo ili kuzisaidia katika uongozi wa nchi hizo na kuzitatulia matatizo yaliyopo. Alisema jambo hilo linabainisha wazi udhaifu wa nchi za Kiislamu hasa kuhusu suala la Palestina. Alisisitiza katika kikao hicho kwamba: “Lau kama nchi za Kiislamu zingesimama kidete na kupambana tangu siku ya kwanza, bila shaka leo hali ya Palestina, eneo la Asia Magharibi na eneo letu ingekuwa tofauti. Leo tungekuwa na nguvu zaidi, umoja zaidi, na hali yetu ingekuwa nzuri zaidi kwa njia tofauti."
Je, ni kwa nini suala la Palestina ni muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu? Na kwa nini linapasa kuwa miongoni mwa masuala na dukuduku za nchi za Kiislamu? Tutajaribu kujibu maswali haya kwa undani kidogo katika vipindi vinavyokuja. Lakini kabla ya hilo, ni muhimu tufafanue masuala kadhaa kuhusu historia na umuhimu wa ardhi ya Palestina, miongoni mwa dini za mbinguni hususan Uislamu.
Ardhi ya Palestina ni chimbuko la dini za mbinguni na Mitume pamoja na Manabii wakubwa wa Mwenyezi Mungu. Ardhi hii ina historia inayorejea nyuma maelfu ya miaka na ni mojawapo ya mahali ambapo ustaarabu wa kwanza wa wanadamu uliundwa. Ardhi ya Palestina inapatikana upande wa magharibi kabisa wa bara la Asia na mashariki mwa bahari ya Mediterania. Nchi hii, inapakana na Lebanon katika upande wa kaskazini, Mto Jordani na Syria upande wa mashariki na Peninsula ya Sinai upande wa kusini, ambayo ni sehemu ya Misri. Katika kipindi chote cha historia yake, ardhi ya Palestina imekuwa ikikaliwa na Waislamu, Wakristo na Mayahudi. Wanaakiolojia wamepata mifupa ya wanadamu wa zamani katika maeneo tofauti ya Palestina, ambapo baada ya kuichunguza kwa makini wametambua kuwa waliishi huko maelfu ya miaka kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as) au kwa jina jingine Yesu Kristo.
Kwa mfano, mabaki ya mwanadamu yalipatikana huko Obeidiyah, karibu kilomita 3 kusini mwa Ziwa Tiberias (Bahari ya Jalil (Galilaya)) huko Palestina, ambayo wanaakiolojia wanaamini kuwa ni ya enzi za Pleistocene, ambacho ni moja ya vipindi vya kijiolojia kutoka miaka milioni 2.5 hadi 10,000 iliyopita. Huenda ni kutokana na sababu hiyo ndipo baadhi ya miji ya Palestina ikachukuliwa kuwa miongoni mwa miji mikongwe zaidi duniani; Miji kama Jericho, Majd na Gaza.
Kutokana na hali yake nzuri ya kijiografia, ustawi wa biashara na kilimo, uhamiaji katika ardhi hii ulianza miaka elfu kadhaa kabla ya kuzaliwa Isah Masih (as). Inaelezwa katika historia ya Palestina kwamba takriban miaka 3500 kabla ya kuzaliwa Masih (as), makabila kadhaa ya Waarabu yalihama kutoka Bara Arabu na kitovu cha Hijaz na kuelekea Palestina. Walikuwa Waarabu Wakanaani. Kwa hiyo, wakazi wa kwanza waliojulikana kihistoria wa Palestina walikuwa Wakanaani, na wakati huo ardhi ya Palestina iliitwa "Ardhi ya Kanaani" kutokana na jina la Waarabu hao. Wakanaani walikuwa wazawa wa Kanaani, mwana wa Sam, mwana wa Nabii Nuhu (as). Walijipatia riziki kupitia kilimo na ufugaji mifugo katika ardhi iliyobarikiwa na nzuri ya Palestina, na kwa kuanzisha mahusiano ya kibiashara na makabila mengine, waliweka misingi ya kwanza ya ustaarabu wa kale. Wakanaani waliohama kutoka Bara Arabu kwenda katika ardhi ya Palestina, walianzisha miji mingi, ukiwemo mji ulioitwa "Yebus". Baadaye, mji huo ulistawi na kupanuliwa na Wafoinike miaka 2500 Kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as) na kubadilishwa jina na kuitwa Ursalem - kwa maana ya amani na urafiki. Kwa hakika, Ursalem ni huohuo mji unaoitwa leo Urshelim kwa lugha ya Kiebrania, au mji wa "Quds" au "Bait al-Maqdis" kwa lugha ya Kiarabu.
Kutokana na nafasi yake nzuri na maalumu ya kijiografia, rutuba ya udongo na utakatifu wake, Palestina daima imekuwa uwanja wa migogoro na mapigano ya udhibiti wake katika historia yake yote. Katika moja ya migogoro na mapigano hayo katika karne ya 13 kabla ya kuzaliwa Masih (as), makabila ya wapiganaji kutoka kisiwa cha Krete na Bahari ya Aegean waliingia Palestina, makabila ambayo jina lao la asili lilikuwa Pelest. Katika maandishi yaliyoachwa na Ramesses III, Firauni wa pili katika kizazi cha 20 cha Misri ya kale, jina la watu hao limetajwa kama "Pulasti", ambalo ni chimbuko la jina la sasa la Palestina. Katika karne ya 12 au 13 kabla ya kuzaliwa Masih (as) BC, makabila hayo yalihamia katika eneo hilo kutoka visiwa vya Bahari ya Aegean (pengine kisiwa cha Krete) na maeneo mengine ya Mediterania, na kuishi katika maeneo ya pwani kati ya Yaffa na Gaza. Kwa mujibu wa Riwaya, miji na vituo vya makazi yao ya awali vilikuwa bandari na miji ya Ashdod, Ashkelon (Asqalon), Gaza, Ekron na Jit.
Inavutia kujua kwamba vyombo vya udongo vimegunduliwa katika eneo hilo ambavyo vilitengenezwa na Wafilisti (Wapulasti) wakiiga utengenezaji wa vyombo vya udongo vya Wagiriki. Nakshi zilizochorwa kwenye vyombo hivyo vya udongo zinaonyesha wazi kwamba Wapulasti walikuwa wapigajani. Walivutiwa sana na dini ya Wakanaani na kuabudu miungu yao (Daigon, Baal na Ishtar). Wapulasti pia walikuwa na ustadi mkubwa katika kuchimba na kutumia madini ya chuma, na hawakuwa na mshindani katika kutengeneza zana za vita vya chuma. Wakati wa shambulio la Yoshua kutoka kabila la Bani Israil lililokusudia kuiteka ardhi hiyo, walipigana na kujitetea vikali kama inavyotajwa mara kadhaa katika kitabu cha Torati.
Wapenzi wasikilizaji, tumefikia mwisho wa kipindi cha leo. Tunakuombeni mjiunge nasi tena katika kipindi kijacho ili tuendelee kuzungumzia historia ya ardhi ya Palestina, nafasi na umuhimu wake kwa ulimwengu wa Kiislamu.