Apr 29, 2024 02:37 UTC

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umeangamiza asilimia 75 ya nyumba, miundombinu ya barabara, vyuo vikuu, misikiti na miundo msingi mingine ya Ukanda wa Gaza.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, Mahmoud Abbas ameitolea wito jamii ya kimataifa na nchi za Ulaya kuitambua rasmi Palestina kama nchi mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa. Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa wito huu katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia. 

Abbas amesema kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel umewashambulia raia wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kuharibu miundombinu yote ya eneo hilo kwa kisingizio cha kulipiza kisasi kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas). 

Abbas: Israel imeangamiza asilimia 75 ya Ukanda wa Gaza 

Mkuu huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utaishambulia Rafah, hayo yatakuwa maafa makubwa zaidi katika historia ya wananchi wa Palestina, na Marekani inapaswa kuizuia Israel kuushambulia mji wa Rafah.  

Akieleza wasiwasi wake kwamba utawala wa Kizayuni utashambulia Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya Gaza, Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, ni lazima kupatikane njia ya ufumbuzi wa kisiasa ili Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu ziweze kujiunga na nchi huru ya Palestina.