Rouhani: Wamarekani hawawezi kuzuia uuzaji mafuta ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani ya kutaka kuzuia mafuta ghafi ya petroli ya Iran yauzwe katika soko la kimataifa na kusema: "Marekani haiwezi kuizuia Iran kuuza mafuta na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itauza mafuta yake."
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo katika mkoa wa Kermansha magharibi mwa Iran wakati wa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo na kuongeza kuwa: "Iran haina uhasama na yeyote na pia haitanyamaza kimya mbele ya njama zozote zile."
Rais Rouhani amesema kujitolea muhanga na nguvu za taifa la Iran ni zaidi ya namna ambayo Wamarekani wanatasawari na kuongeza kuwa: "Iran itajibu uhasama na njama kwa muqawama."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesisitiza kuwa, uhusiano wa Iran na nchi jirani ni mzuri sana na kuongeza kuwa: "Wairani watamfanya adui ajute na kurejea katika mantiki."
Rais Rouhani aidha ameashiria kuzinduliwa miradi kadhaa ya maendeleo kwa wakati mmoja katika mikoa 13 ya Iran hii leo na kusema: "Wakati adui anapoonyesha kiburi na kutoa matamshi yasiyo na maana na ghalati, kunazinduliwa miradi hii ambayo inatoa pigo kwa huyo adui."
Leo katika safari ya Rais Hassan Rouhani mkoani Kermanshah kulizinduliwa miradi mbali mbali ya maendeleo katika mikoa 13 kote Iran.