May 09, 2019 09:26 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; Ulimwengu wavutiwa na mafundisho ya kidini

Huku akiashiria hitajio muhimu la wamadamu wa leo kuhusiana na mafundisho ya dini na vilevile hamu inayoonyeshwa na Ulimwengu wa Kiislamu na hata jamii zisizokuwa za Kiislamu kuhusu suala hilo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, leo jukumu la vyuo vya kidini ni zito zaidi ikilinganishwa na huko nyuma.

Akizungumza Jumatano alasiri mbele ya wanafunzi, wanazuo, wahadhiri na wakuu wa vyuo vya kidini kutoka pembe zote za nchi, Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba vyuo hivyo ni vituo ambapo wanazuoni wa kidini hupata malezi ya kuwawezesha kuingia katika uwanja wa kueneza Uislamu huku wakiwa wamejizatiti vilivyo na maarifa ya Kiislamu.

Wanafunzi na wanazuoni katika nchi za Kiislamu wana nafasi muhimu katika kuarifisha na kueneza misingi ya mafundisho ya Kiislamu na kuhusu hilo, nafasi ya vyuo vya kidini au kwa jina jingine Hauza, ni muhimu zaidi kuliko taasisi nyigine za Kiislamu. Juhudi zinazofanywa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuzuia kuenezwa mafundisho ya dini na maadili ya Kiislamu katika jamii ni jambo linalotoa udharura wa kuimarishwa juhudi za kulea wanafunzi, maulamaa na wanafikra wa Kiislamu kwa ajili ya kuzima njama hiyo hatari ya Wamagharibi. Maadui wa Uislamu wanatumia kila mbinu kuhakikisha kwamba wanawatenganisha Waislamu na misingi ya mafundisho yao ya kidini ili kuwafanya wawe sawa na jamii za Kimagharibi ambazo zinazingatia tu masuala ya kimaada na kidunia. Jamii hizo za kimaada za Magharibi hazizingatii hata kidogo imani na misingi ya dini ya Kiislamu na daima zinafanya juhudi za kudhoofisha na kisha kuharibu kabisa nafasi ya wanaolinda misingi hiyo ya dini.

Ayatullah Khamenei akizungumza mbele ya wanafunzi, wahadhiri, wanazuoni na wakuu wa vyuo vya kidini

Katika hali hiyo nafasi ya viongozi wa kidini na wanazuoni katika kujenga utambulisho na utamaduni wa kidini na kimaadili wa wanadamu katika jamii ya Kiislamu na jamii nyinginezo ni jambo lenye umuhimu usiokanushika. Kwa kutilia maanani majukumu yake ya dhati, vyuo vya kidini vina nafasi muhimu mno katika kubainisha na kueneza mafundisho ya Kiislamu na kidini katika jamii za Kiislamu na zisizo za Kiislamu, kupitia manafunzi na wanafikra wa Kiislamu wanaolelewa katika vyuo hivyo. Kwa mfano, hatuwezi kuilinganisha jamii ya sasa ya Iran na ile ya kipindi cha utawala wa taghuti Shah kuhusiana na suala zima la kuimarisha na kueneza mafundisho ya dini, kwa kuzingatia kuwa katika jamii ya Kiislamu ya leo hapa nchini, suala hilo limebadilishwa na kuwa utamaduni na msingi muhimu katika maisha ya kila siku ya Wairani.

Mambo kama vile utamaduni wa Kiirani - Kiislamu, ustaarabu wa Kiirani - Kiislamu na maisha ya Kiirani - Kiislamu ni suala lililokita mizizi nchini kutokana na juhudi zilizofanywa na vyuo vya kidini, wanafunzi na wanazuoni.

Katika uwanja huo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduziya Kiislamu amevitaja vyuo hivyo vya kidini kuwa vituo vya kutoa mafundisho ya Kiislamu na kuyaimarisha katika jamiin a kuongeza kuwa: Kuwafundisha watu mafundisho ya dini ni sehemu moja ya majumuku ya vyuo vya kidini na sehemu nyingine ya majukumu hayo ni kueneza na kuthibitisha mafundisho hayo katika maisha ya watu.

Baadhi ya wanafunzi na wanazuoni waliokutana na Kiongozi Muadhamu

Ushirikiano na mawasiliano mazuri yaliyopo kati ya vyuo hivyo vya kidini na vyuo vikuu vya kawaida yameimarisha zaidi taathira ya wanafunzi wa masomo ya kidini na wanazuoni katika jamii. Wanafunzi na wanazuoni hao kutoa majibu sahihi na ya kimantiki kwa maswali yanayoulizwa na matabaka mbalimbali ya jamii na hasa tabaka la vijana, kumezuia uwezekano wa watu kujihusisha na mambo yasiyo na faida yoyote kiimani na kimaanawi. Kufuatilia mambo hayo matupu na ya kimaada kwa sasa ni changamoto kubwa inayozitatiza jamii za nchi za Magharibi. Kuchoshwa vijana wa jamii hizo na jambo hilo na hatimaye kuchukua uamuzi wa kuelekea upande wa mafundisho ya kidini ni jambo linalothibitisha wazi kwamba jamii zilizo nje ya Ulimwengu wa Kiislamu pia zimeanza kuvutiwa na mafundisho hayo ya kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitiza suala hilo kwa kusema: Dhana kwamba watu katika pembe mbalimbali za dunia wamechoswa na mafundisho ya kidini ni dhana potovu, bali hamu yao ya kupata mafundisho hayo imeongezeka zaidi.

Tags