Zarif: Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani umewalenga wananchi wa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, ugaidi wa kiuchumi wa Marekani umewalenga wananchi wa Iran.
Dk Mohammad Javad Zarif aliandika jana usiku kwenye ukurasa wake wa mtandao huo wa kijamii kwamba vita na mazungumzo ni vitu ambavyo haviwezi kwenda sambamba iwe ni kwa masharti au bila ya masharti. Dk Zarif ameweka pia mkanda wa video kwenye ukurasa wake huo wa Twitter kuhusiana na mtoto wa Kiirani anayehitajia mguu bandia huku familia yake ikiwa haina uwezo wa kumdhaminia mtoto wao mguu huo wa kumsaidia kutembea.
Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema pia katika mahojiano na shirika la habari la ABC News kwamba, 'mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani' yanawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na kwamba Tehran itatoa jibu mwafaka katika kujihami na ugaidi huo wa Marekani.
Bila kutoa maelezo ya kina kuhusu taathira zenyewe, Dakta Zarif ameeleza kuwa, "Iwapo Marekani itawasababishia Wairani maumivu makali kutokana na vita vyake vya kiuchumi sambamba na kuielekezea Iran ugaidi wa kiuchumi, bila shaka matokeo ya jambo hilo yatakuwa mabaya."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kwa kusema: "Sisi hatutofautishi kati ya vita vya kiuchumi na vita vya kijeshi."