Iran yakosoa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya sekta yake ya petrokemikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53988-iran_yakosoa_vikwazo_vipya_vya_marekani_dhidi_ya_sekta_yake_ya_petrokemikali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hatua ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuliwekea vikwazo shirika moja la petrokemikali la Iran.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jun 08, 2019 02:20 UTC
  • Iran yakosoa vikwazo  vipya vya Marekani dhidi ya sekta yake ya petrokemikali

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hatua ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuliwekea vikwazo shirika moja la petrokemikali la Iran.

Katika taarifa,  leo Jumamosi, Sayyid Abbas Mousavi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani haitafikia malengo yake katika vikwazo dhidi ya Iran. 

Siku ya Ijumaa Wizara ya Fedha ya Marekani ilitoa taarifa ikisema imeweka vikwazo dhidi ya shirika moja la petrokemikali la Iran linalojulikana kama Persian Gulf Petrochemical Industries Company. Aidha taarifa hiyo imesema mashirika mengine 39 yanayofungamana na shirika hilo nayo pia yako katika orodha ya vikwazo.

Kufuatia hatua hiyo, Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema sera za Marekani za kuiwekea Iran mashinikizo ya juu zaidi ni sera zilizofeli na hata rais aliyetangulia katika nchi hiyo alipata uzoefu huo wa kufeli. Ameongeza kuwa: "Hatua mpya ya Wizara ya Fedha ya Marekani katika kuyawekea vikwazo mashirika ya petrokemikali ya Iran ni sawa na ugaidi wa kiuchumi na ni muendelezo wa sera za Ikulu ya White House dhidi ya taifa la Iran.

Kiwanda cha petrokemikali

Mousavi amesisitiza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kinyume cha misingi ya uhusiano na sheria za kimataifa. Ameongeza kuwa, nchi zote zinawajibika kutoa jibu kwa ukiukwaji huu wa wazi wa misingi ya sheria za kimataifa na zisiruhusu mafanikio ya jamii ya kimataifa katika uga wa maamuzi ya pande kadhaa yaharibiwe na sera za Marekani za maamuzi ya upande moja.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ameashiria madai ya baadhi ya wakuu wa Marekani kuhusu kutaka kufanya mazungumzo na Iran na kusema madai hayo ni hadaa tupu na hayana uhakika na yanatolewa tu kwa ajili ya kuvutia fikra za umma Marekani. Amesema haijapita wiki moja na imebainika kuwa madai hayo ya rais wa Marekani ya kutaka mazungmzo na Iran ni hadaa tupu.