Waziri Mkuu wa Japan afanya ziara ya kihistoria nchini Iran + Video
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54080-waziri_mkuu_wa_japan_afanya_ziara_ya_kihistoria_nchini_iran_video
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo jioni amempokea rasmi Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe aliyepo hapa nchini kwa ziara rasmi ya kihistoria ya siku mbili. Mapokezi hayo rasmi yamefanyika katika Ikulu ya Sa'dabad hapa Tehran.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 12, 2019 11:16 UTC
  • Waziri Mkuu wa Japan afanya ziara ya kihistoria nchini Iran + Video

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo jioni amempokea rasmi Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe aliyepo hapa nchini kwa ziara rasmi ya kihistoria ya siku mbili. Mapokezi hayo rasmi yamefanyika katika Ikulu ya Sa'dabad hapa Tehran.

Hii ni ziara ya kwanza ya Waziri Mkuu wa Japan nchini Iran katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita na moja ya malengo ya safari yake hiyo ni kupunguza wasiwasi uliopo baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani. Waziri Mkuu wa Japan amewasili hapa nchini Iran mapema leo asubuhi.

Televisheni ya Press TV imesema kuwa, mbali na kuonana na Rais Rouhani, Shinzo Abe anatarajiwa kuonana na kufanya mazungumzo pia na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kesho Alkhamisi.

 

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu wa Japan imefanyika hapa Tehran baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kuitembelea Japan na kumuomba Shinzo Abe afanye ziara nchini Iran kama juhudi za kupunguza wasiwasi uliopo baina ya Washington na Tehran uliosababishwa na Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya mapatano hayo muhimu ya kimataifa. 

Si hayo tu lakini pia serikali ya Marekani imeiwekea Iran vikwazo ambavyo Washington inajigamba kuwa ni vikubwa zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya nchi fulani, na wakati huo huo Trump anadai kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Iran bila ya masharti yoyote. 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Trump ameelekeza tamaa zake kwa ziara hiyo ya Waziri Mkuu wa Japan hapa Iran ili kuondoa mkwamo uliosababishwa na siasa mbovu za serikali yake huko Marekani.