Ayatullah Khatami: Taifa la Iran halitafanya mazungumzo kutokana na mashinikizo
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema kuwa kufanya mazungumzo na Marekani hakuna faida yoyote, na taifa la Iran kamwe halitafanya mazungumzo chini ya mashinikizo ya kiuchumi.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema kuwa, Marekani itaingia kaburini na kuzikwa na matarajio yake ya kutaka kufanya mazungumzo na Iran na kuongeza kuwa: Watawala wa Marekani na pembetatu za Donald Trump, John Bolton na Mike Pompeo si wakweli na madai kuwa wako tayari kufanya mazungumzo na Iran ni uongo mtupu, kwa sababu Trump anataka kupata kura za Warekani katika uchaguzi ujao wa rais kwa kuivuta Iran katika meza ya mazungumzo.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema Iran haitakariri yaliyotokea katika mazungumzo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Matamshi ya Kiongozi Muadhamu Ayatullah Ali Khamenei katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe yalikuwa na mantiki na busara; na kutokubali kwake ujumbe wa Rais wa Marekani ni aina fulani ya kumdhalilisha Trump mwenye kiburi. Ayatullah Khatami amesema madai ya Trump kwamba Marekani haina nia ya kuuondoa madarakani utawala wa Kiislamu nchini Iran ni uongo mkubwa kwa sababu katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita marais wote waliotawala Marekani walishindwa kufanya hivyo.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria mauaji ya kizazi yanayofanywa nchini Yemen na utawala wa kiukoo wa Saudi Arabi na kusema: Jina la utawala wa kizazi cha Aal Saud linaonekana popote pale kunapozungumziwa mauaji na uporaji, na utawala huo umeua maelfu ya watoto na wanawake wa Yemen kwa kuharibu miundombinu ya nchi hiyo.
Kuhusu hiyama na msaada wa Saudi Arabia na Imarati kwa Baraza la Kijeshi la Sudan katika kuua rai wanaoandamana kwa amani nchini humo Ayatullah Khatami amesema: Kunyongwa kwa wapinzani nchini Saudia wakiwemo watoto pia ni kielelezo cha utambulisho na dhati ya utenda jinai na umwagaji damu wa utawala wa Saudi Arabia.