Apr 20, 2016 03:39 UTC
  • Zarif na Kerry wajadili njia za kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Marekani wamekutana na kuzungumzia njia za kuhakikisha makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Jamhuri ya Kiislamu na madola sita makubwa duniani yanatekelezwa kama ilivyoafikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, wamekubaliana kuwa kuna ulazima wa kutekelezwa ipasavyo makubaliano ya nyuklia kama ilivyopangwa ili kuhakikisha yananufaisha pande zote mbili husika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York mara baada ya mazungumzo hayo, Kerry amesema wamekubaliana kuhakikisha makubaliano ya nyuklia yanatekelezwa kwa namna itakayonufaisha pande zote kama ilivyokubaliwa. Ameongeza kuwa watafanya kikao kingine siku ya Ijumaa pembeni ya hafla ya kusaini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi itakayofanyika Paris, Ufaransa.

Katika mazungumzo hayo ya pamoja na waandishi wa habari Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema wamejadili njia zitakazohakikisha Jamhuri ya Kiislamu inanufaika na yale ambayo ni haki yake kulingana na utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia.

Mwaka uliopita, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 zilifikia makubaliano ya nyuklia ambayo utekelezaji wake ulianza miezi mitatu nyuma.

Hata hivyo mchakato wa "ufunguaji njia za kiuchumi" kwa ajili ya Iran umekuwa ukipiga hatua kwa mwendo wa kujikongoja, kutokana na Jamhuri ya Kiislamu kushindwa kufanya miamala na mabadilishano ya nje kwa kutumia sarafu ya dola na vilevile kuendelea kuwa na wasiwasi benki kubwa za kigeni kufanya miamala ya kifedha na Tehran.../

Tags