May 06, 2021 12:49 UTC
  • Zarif: Palestina ni kipimo cha haki; Iran imesimama na Wapalestina kwa fahari

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Palestina ni kigezo na kipimo cha haki na uadilifu, lakini ni nchi chache zimeweza kupasi katika kipimo hicho.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo Alkhamisi katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds itakayoadhimishwa kesho Ijumaa.

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kwa fakhari kubwa imesimama bega kwa bega na wananchi wa Palestina, ambao wamesimama kidete kupinga dhulma na ukandamizaji wa utawala wa kibaguzi (apartheid).

Dakta Zarif ameongeza kuwa, Siku ya Quds ni kumbusho la kila mwaka la wajibu wa kiakhlaqi wa dunia kusimama kuwatetea Wapalestina.

Ikumbukwe kuwa, Imam Khomeini MA, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ramadhani ya mwaka 1979 alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds.

Waislamu na wapenda haki wamekuwa wakifanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds tokea wakati huo, na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 katika aghalabu ya maeneo ya dunia hakutafanyika mijumuiko hadharani katika Siku ya Kimataifa ya Quds bali kutakuwepo zaidi na harakati katika mitandao ya kijamii zikiwemo hotuba za shakhsia mbali mbali.

Tags