Mar 17, 2021 06:34 UTC
  • Iran yakosoa undumakuwili wa Uingereza, yataka silaha zote za nyuklia ziharibiwe

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali undumakuwili wa Uingereza; ambayo kwa upande mmoja inatoa madai yasiyo na msingi dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani na kwa upande mwingine, inasema kuwa inataka kuongeza akiba ya silaha zake za nyuklia.

Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumanne katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter na kubainisha kuwa: Katika undumakuwili wa kupindukia, Waziri Mkuu wa Uingereza Borris Johnson anadai eti anatiwa wasiwasi na uwezekano wa Iran kuunda silaha ya nyuklia, na siku hiyo hiyo anatangaza kuwa nchi yake inataka kuongeza kiwango cha silaha za nyuklia inachomiliki.

Katika ujumbe huo wa Twitter, Dakta Zarif ameongeza kuwa: Kinyume na Uingereza na waitifaki wake, Iran inaamini kuwa silaha za nyuklia na silaha nyinginezo za maangamizi (WMDs) ni za kikatili na zinapaswa kuangamizwa. Uingereza hivi sasa inamiliki vichwa 180 vya nyuklia, kinyume na 500 ilivyokuwa navyo wakati wa kupamba moto Vita Vikuu Vya Pili ya Dunia katika miaka ya 1970.

UK imetangaza nia yake kuongeza kiwango cha silaha zake za nyuklia katika hali ambayo, mara kadhaa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza kuwa, nchi hii haijawahi kuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia wala kuzitumia.

Silaha za maangamizi za nyuklia

Mwezi uliopita, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema, "Kama ambavyo tumesema mara kadhaa, silaha za maangamizi ya umati, zikiwemo silaha za nyuklia, hazina nafasi yoyote katika mpango wa nchi hii wa kiulinzi na huu ndio msimamo thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu.  

Iran ni mwanachama wa mkataba wa NPT wa kuzuia uundwaji na usambazwaji silaha za nyuklia na pia inashirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Atomiki IAEA na imetekeleza maagizo ya wakala huo kuhusiana na usalama wa miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya kiraia.

Tags