Zarif: Enzi za ukiritimba wa Wamagharibi duniani zimekwisha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria juu ya kuimarika nafasi chanya ya mataifa ya Asia duniani na kueleza bayana kuwa, ukiritimba wa nchi za Magharibi katika uhusiano wa kimataifa umefikia ukingoni.
Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumatatu katika mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu wa Sekritarieti ya Jukwaa la Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Asia (CICA) na kubainisha kuwa, enzi za ukiritimba na utawala wa Magharibi katika mfumo wa dunia zimekwisha.
Dakta Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kwa dhati jitihada zozote za kujenga muamana na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa jukwaa la CICA.
Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameipongeza Kazakhstan kwa nafasi yake katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na vile vile mazungumzo ya amani ya Syria ya Astana akisisitiza kuwa, huo ndio mchakato pekee athirifu wa kurejesha amani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kwa upande wake, Kairat Sarybay, Mkurugenzi Mkuu wa Sekritarieti ya Jukwaa la Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Asia (CICA) amegusia kuhusu nafasi na mchango wa Iran katika masuala kieneo na pia amemdokeza Dakta Zarif kuhusu mipango na mikutano ijayo ya ngazi ya mawaziri wa nchi wanachama wa CICA.
Jukwaa la Maingiliano na Hatua za Kujenga Hali ya Kuaminiana Asia (CICA) liliasisiwa mwaka 1992, na hivi saa lina nchi wanachama 27 pamoja nchi nane watazamaji.