Apr 13, 2021 06:56 UTC
  • Zarif: Kukishambulia kituo cha nyuklia cha Iran ni jinai ya kivita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kitendo cha Jumapili alfajiri cha kushambuliwa kwa makusudi mfumo wa usambazaji umeme wa kituo cha urutubishaji urani cha kituo cha nyuklia cha Natanz hapa nchini ni jinai ya kivita.

Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika barua aliyomuandikia Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo amelaani na kulalamikia vikali kitendo hicho cha kigaidi kilichofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika barua hiyo, Dakta Zarif amesema wanasayansi na wahudumu wengine wachapakazi wa kituo hicho cha nyuklia cha Shahid Mostafa Ahmadi Roshan walichukua hatua za dharura na haraka kuzuia kutokea madhara makubwa na hatarishi kwa binadamu na mazingira kutoka na shambulio hilo.  

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesisitizia udharura wa kulindwa taasisi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran, kwani kituo cha nyuklia cha Natanz huko nyuma pia kiliwahi kushambuliwa kimtandao kwa ushirikiano wa Marekani na utawala wa kigaidi wa Israel.

Wanasayansi shupavu wa Iran katika kituo cha nyuklia cha Natanz

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kanuni za kulinda usalama wa vituo vya nyuklia pamoja na maazimio ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, ni marufuku kuchukua hatua za uharibifu na mashambulio ya kimtandao dhidi ya taasisi za nyuklia za nchi nyingine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, kitendo hicho cha Wazayuni ni mchezo wa pata potea wa kipumbavu na kwamba iwapo Marekani inataka kuzuia matokea mabaya ya ushenzi huo, basi iharakishe kuliondolea taifa hili vikwazo vya kidhalimu. 

Tags