Iran yaonyesha mabaki ya Drone ya Marekani iliyotunugliwa
Iran imeonyesha mabaki ya ndege isiyo na rubani (drone) ya kijasusi ya Marekani ambayo ilitunguliwa mapema Alhamisi baada ya kikuka anga ya Iran.
Kamanda wa Kitengo cha Angani cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amehutubia waandishi habari wakati wa kuonyesha mabaki ya drone hiyo. Amesema drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilionywa mara kadhaa baada ya kukiuka anga ya Iran na kwamba onyo la mwisho lilitolewa 9:55 Alhamisi alfajiri, dakika 10 kabla ya kutunguliwa.
Amesema pamoja na kuwa ndege hiyo haikuwa na rubani lakini ina mfumo wa kupokea ujumbe na kuutuma katika makao makuu. Brigedia Jenerali Hajizadeh amesisitiza kuwa usalama wa taifa ni mstari mwekundu wa Majeshi ya Iran.
Aidha ametoa maelezo kamili kuhusu harakati za drone hiyo ambayo ilianza shughuli zake za ujasusi saa sita na dakika 14 mapema Alhamisi ikitokea katika uwanja mmoja wa ndege za kivita katika Umoja wa Falme za Kiarabu kabla ya kutunguliwa 10:05 karibu na Kouh-e-Mobarak katika eneo la Jask mkoani Hormozgan kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Iran imetoa za mfumo wa kiimataifa wa GPS, drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilikuwa katika anga ya Iran wakati wa kutunguliwa. Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti drone hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa.