Rouhani: Uingiliaji wa kijeshi wa Marekani ni chanzo cha matitzo katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54301-rouhani_uingiliaji_wa_kijeshi_wa_marekani_ni_chanzo_cha_matitzo_katika_eneo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera za Iran ni kupunguza taharuki, kujiweka mbali na kila aina ya makabiliano ya kijeshi sambamba na kueneza amani na uthabiti katika eneo na dunia nzima.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2019 08:42 UTC
  • Rouhani: Uingiliaji wa kijeshi wa Marekani ni chanzo cha matitzo katika eneo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera za Iran ni kupunguza taharuki, kujiweka mbali na kila aina ya makabiliano ya kijeshi sambamba na kueneza amani na uthabiti katika eneo na dunia nzima.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumapili mjini Tehran wakati alipokutana na Gabriela Cuevas Barron,  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia (IPU). Rais wa Iran ameongeza kuwa, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ni tatizo kubwa hivi sasa katika uga wa kimataifa na kuongeza kuwa: "Chimbuko la matatizo ya kieneo na dunia ni udikteta wa baadhi ya nchi hasa Marekani ambazo zimekuwa zikikiuka kanuni za kimataifa na mchakato wa maamuzi ya pande kadhaa."

Rais wa Iran ameashiria hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: "Leo Marekani inatumia ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran na hata imeweka vikwazo katika sekta za dawa na vyakula."

Rais Rouhani amesema Marekani imesababisha matatizo na migogoro katika eneo kutokana na uingiliaji wake wa kijeshi na kuongeza kuwa:"Hatua ya drone (ndege isiyo na rubani) ya Marekani kukiuka anga ya Iran ni mwanzo wa taharuki mpya ya Marekani katika eneo na ni tishio kwa usalama wa njia muhimu ya baharini ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman." Rais wa Iran pia amesema taasisi za kimataifa zinapaswa kutoa jibu linalofaa kwa hatua hiyo ya kichokozi ya Marekani.

Sehemu ya mabaki ya drone ya Marekani aina ya  RQ-4A Global Hawk, inayogharimu dola milioni 220 ambayo ilitunguliwa Alhamisi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kukiuka anga ya Iran

Rais wa Iran aidha ameashiria uingiliaji wa Marekani nchini Afghanistan, Iraq, Syria na Yemen katika kipindi cha miaka 17 iliyopita na kusema: "Usalama wa Ghuba ya Uajemi unapaswa kudhaminiwa na nchi za eneo kama ambavyo usalama wa maeneo mengine yote duniani nao pia unapaswa kudahminiwa tu na nchi za maeneo hayo."

Kwa upande wake, Gabriela Cuevas Barron,  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabunge ya Dunia (IPU ameashiria nafasi muhimu ya Iran katika kuhimiza maamuzi ya pande kadhaa na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na kusema: "Mapatano ya JCPOA yameonyesha maamuzi ya pande kadhaa ni muhimu katika kuleta amani na usalama kieneo na duniani."  Amesema uzoefu wenye mafanikio wa Iran unapaswa kutumiwa katika kutatua matatizo ya kimataifa kupitia mazungumzo sambamba na kuheshimiwa mapatano ya kimataifa.