Rais Rouhani: Iran haitaki vita na mapigano Ghuba ya Uajemi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran haitaki vita na mapigano katika eneo la Ghuba ya Uajemi lakini haitaruhusu maadui kuvuka mipaka yake kinyume cha sheria.
Rais Rouhani ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Mawazi ambako ameashiria tukio la ndege ya ujasusi isiyo na rubani ya Marekani iliyoingia katika anga ya Iran kinyume cha sheria na kusema: Kama adui atafanya uchokozi na kuvuka mipaka ya Iran kinyume cha sheria atakuwa amevuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu, na Iran itatoa jibu kali kwa hatua kama hiyo.
Rais Hassan Rouhani amesema kuwa mfumo wa makombora uliotengenezwa kikamilifu hapa Iran umetungua na kuangusha ndege ya ujasusi isiyo na rubani ya Marekani na kuongeza kuwa: Iran imepata maendeleo katika elimu, sayansi, viwanda na sekta ya kijeshi na isiyo ya kijeshi.
Vilevile ameashiria siasa zilizo dhidi ya Iran za serikali ya Marekani na kusema: Katika siku hizi Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, imechanganyikiwa na hotuba na matamshi yanayotolewa na maafisa wake hayafai na yanachekesha.
Rais Rouhani ameashiria madai yaliyotolewa na Rais wa Marekani kwamba ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa Iran kupata silaha za nyuklia na kusema: Kama Donald Trump ana wasiwasi kuhusu Iran kupata silaha za nyuklia kwa nini ananyamaza kimya mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unamiliki silaha nyingi za nyuklia?
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema, kwa mujibu wa fatwa iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia, Tehran haina nia ya kuwa na silaha za nyuklia. Ameongeza kuwa, Wamarekani wenyewe wamethibitisha kuwa maneno yao hayana msingi na ni uongo.
Rais Rouhani amesema Wamarekani na Ulaya wamechagua njia isiyo sahihi kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na amewaasa washikamane na kutekeleza ahadi na majukumu yao.