Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: Umma wa Kiislamu umeshuhudia ushindi mtawalia
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo Tehran amesema umma wa Kiislamu umeshuhudia mfufulizo wa ushindi na mafanikio licha ya vikwazo visivyo vya kiadilifu vya Marekani.
Hujjatul Islam Mohammad Hassan Abutorabi Fard amesema hayo katika hotuba zake za Sala ya Ijumaa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyoshuhudiwa hivi karibuni katika ulimwengu wa Kiislamu, ni umma kusimama kidete dhidi ya mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne."
Amesema harakati za muqawama za Palestina zimeweka pembeni tofauti zao na kwa sauti moja zimepinga njama hizo za Marekani na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo Tehran ameashiria hatua ya kutunguliwa ndege isiyo na rubani (drone) ya Marekani ambayo ilikuwa imekiuka anga ya Iran na kusema, "Ushirikiano baina ya vituo vya sayansi (Vyuo Vikuu) na Wizara ya Ulinzi unapaswa kuimarishwa zaidi. Kuitungua drone ya kisasa kabisa ya Marekani ni ujumbe kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuzima uvamizi na chokochoko zozote dhidi yake.
Wiki iliyopita, drone ya kijasusi ambayo Wamarekani walikuwa wanadai kuwa haiwezi kuonekana kwenye rada huku wakiinadi kuwa iliyo ya kisasa zaidi duniani aina ya Global Hawk, ililengwa na kutunguliwa kwa ustadi mkubwa na makombora yaliyotengenezwa nchini Iran.
Kadhalika Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo Tehran amepongeza hatua ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, kukataa kupokea wala kujibu ujumbe wa Rais Donald Trump, na kusisitiza kuwa kitendo hicho kimeupa izza umma wa Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Hujjatul Islam Mohammad Hassan Abutorabi Fard amezitaka taasisi za serikali hapa nchini kufuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu, ya kuhakikisha kuwa taifa hili linapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa pato la mafuta katika kuendesha mambo yake, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kumekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa nchi.