Ayatullah Kermani: Marekani inaogopeshwa sana na uwezo wa kiulinzi wa Iran
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amejibu matamshi ya rais wa Marekani juu ya sababu iliyoifanya Washington kujiepusha kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, viongozi wa Marekani wanaogopa uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Iran.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi-Kermani ameyasema hayo katika hotuba ya Sala ya Ijumaa ya hapaTehran na amegusia pia kumbukumbu za kushambuliwa ndege ya abiria ya Iran na meli ya kivita ya Marekani ya USS Vincennes tarehe 3 Julai 1988 na kuongeza kuwa, Marekani ilitenda jinai hiyo kwa ufidhuli, bila haya na kwa makusudi. Akibainisha kwamba viongozi wa Marekani wamepatwa na woga amesema kuwa, Wairan wanawaonyesha walimwengu uwezo wao mkubwa kwa kutumia uelewa wao, akhlaqi na ubinaadamu. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuvuka kiwango kilichoainishwa na JCPOA cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa na kusema kuwa, Tehran haina haja na silaha za maangamizi ya umati kwa kuwa inatambua kwamba kuunda silaha hizo ni haramu.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi-Kermani amesema kuwa Iran ndiyo yenye haki ya kujiainishia kiwango cha urutubishaji urani baada ya nchi za Ulaya kutotekeleza ahadi zao katika mapatano ya JCPOA. Ameongeza kuwa Tehran itaongeza kiwango inachokihitaji cha urani iliyorutubishwa kwa ajili ya matumizi ya kielimu na kudhamini nishati yake. Aidha ameashiria kwamba Wazayuni wanaishi kwenye nyumba ya vioo na kusisitiza kuwa, iwapo Marekani na Wazayuni watafanya kosa hata kidogo, basi Iran italigeuza eneo la Ghuba ya Uajemi kuwa kaburi la Wamarekani. Aidha baada ya Sala ya leo Ijumaa, Waislamu nchini Iran wamepiga nara kulaani siasa za uhasama za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kusisitizia udharura wa kusimama imara na muqawama kwa ajili ya kuzishinda njama za maadui.