Rais Rouhani: Waingereza ndiyo walioanzisha ukosefu wa amani baharini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54675-rais_rouhani_waingereza_ndiyo_walioanzisha_ukosefu_wa_amani_baharini
Rais wa jamhuri ya kiislamu ya Iran amesema kuwa hatua ya Uingereza ya kusimamisha meli ya mafuta ya Iran ni ya kitoto sana, kipumbavu na ni makosa na kwamba Waingereza ndio walioanzisha machafuko na ukosefu wa amani baharini na watakuja kuona athari zake mbaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2019 07:03 UTC
  • Rais Rouhani: Waingereza ndiyo walioanzisha ukosefu wa amani baharini

Rais wa jamhuri ya kiislamu ya Iran amesema kuwa hatua ya Uingereza ya kusimamisha meli ya mafuta ya Iran ni ya kitoto sana, kipumbavu na ni makosa na kwamba Waingereza ndio walioanzisha machafuko na ukosefu wa amani baharini na watakuja kuona athari zake mbaya.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa, Uingereza imechukua hatua ya kusimamisha na kuzuia meli ya mafuta ya Iran kwa niaba ya kundi "B" yaani Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Zayed ambaye ni mrithi wa kiti cha mtawala wa Imarati na John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani. Ameongeza kuwa, Waingereza wamesimamisha na kuzuia meli ya mafuta ya Iran katika eneo la Jabal Tariq (Gibraltar) ambako wao wenyewe ni wavamizi. 

Rais Rouhani amesema kuwa, pande zote zinapaswa kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba, njia za usafiri wa meli baharini zinakuwa salama kote duniani kwa sababu kukaririwa kwa hatua kama hii ya Uingereza kutavuruga amani na usalama duniani na kusababisha hasara kwa pande zote.

Rais Rouhani katika baraza la mawaziri, Tehran

Rais Rouhani ameitaja hatua ya Marekani ya kulitaka Baraza la Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuchungua hatua ya Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni kichekesho kisichokuwa na kifani na kusema: Katika upande mmoja Wamarekani wanasema makubaliano ya JCPOA ndiyo mabaya zaidi katika historia na wamejiondoa katika makubaliano hayo bila sababu yoyote, na katika upande wa pili Iran inapopunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo wanasema hatua hiyo inatia wasiwasi! 

Amesisitiza kuwa hatua ya Iran imechukuliwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya JCPOA na kuongeza kuwa, Iran ilizipatia nchi za Ulaya fursa ya siku 60 na sasa na imezipa fusra nyingine ya miezi miwili kwa hatua yake mpya.  

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mwenendo wa kupunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA utaendelea na amehoji kwamba, je urutubishaji wa madini ya urani ambayo yanatumiwa katika mambo mengi kwa malengo ya amani katika masuala ya teknolojia ni mbaya kwa Iran lakini mzuri kwa mataifa mengine?