Wanachuo wakusanyika mjini Mashhad kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54956-wanachuo_wakusanyika_mjini_mashhad_kumuunga_mkono_sheikh_ibrahim_zakzaky
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ferdowsi cha mjini Mashhad kaskazini masharikki wa Iran wamefanya mkusanyiko mkubwa na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 24, 2019 04:15 UTC
  • Wanachuo wakusanyika mjini Mashhad kumuunga mkono Sheikh Ibrahim Zakzaky

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ferdowsi cha mjini Mashhad kaskazini masharikki wa Iran wamefanya mkusanyiko mkubwa na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Wanachuo hao sambamba na kupiga nara za kulaani ukandamizaji dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky wametoa wito wa kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu.

Mkusanyiko huo wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Ferdowsi mjini Mashhad unafanyika sambamba na kushadidi maandamano na mashinikizo dhidi ya serikali ya Nigeria yanayotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Wakati huo huo, wasomi mashuhuri 52 na wanaharakati wamemwandikia barua ya wazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakimtaka achukue hatua za haraka za kuhakikisha kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mwewe Malam Zeenat, wanapatiwa matibabu. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria

Mwaka 2015, jeshi la Nigeria lilivamia na kushambulia mkusanyiko wa Waislamu katika Husseiniyah ya Baqiyatullah huko Zaria kwenye jimbo la Kano na kuua shahidi karibu Waislamu elfu moja. 

Sheikh Zakzaky mwenyewe na mkewe walipigwa risasi na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammadu Buhari ambayo inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumwachilia huru mwanachuoni huyo.