Rouhani: Marekani imepoteza matumaini ya kuvunja uhuru wa taifa la Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani imepoteza matumaini ya kuvunja na kusambaratisha uhuru wa taifa la Iran.
Rais Rouhani ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika sherehe za mwaka wa 39 wa kuasisiwa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ambapo ameashiria vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran na kuongeza: "Wasomi na wataalamu Wairani wanaweza kubadilisha vikwazo kuwa fursa."
Rouhani pia amesema mafanikio ya Iran katika kutungua ndege isiyo na rubani (drone) ya kijasusi ya Marekani ni ishara ya umahiri wa Kiirani na kuongeza kuwa: "Kutunguliwa drone ya kijasusi ya Marekani tena kwa kutegemea zana zilizoundwa Iran ni jambo la fahari."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran inataka kuamiliana vizuri na dunia lakini yeyote atakayekiuka mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atapata jibu kali.
Itakumbukwa kuwa siku ya tarehe 20 Juni ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya Marekani aina ya Global Hawk ilitunguliwa na kuteketezwa na kikosi cha anga za mbali cha IRGC baada ya kuvuka mpaka wa anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.