Rouhani: India na Pakistan zivute subira ili kuzuia machafuko huko Kashmir
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan kwamba: Iran inazitolea wito India na Pakistan zizuie machafuko na kuuliwa watu wasio na hatia katika eneo la Kashmir kwa pande mbili hizo kuwa na subira na uvumilivu.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumapili katika mazungumzo yake ya simu na Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan na akasema usalama wa eneo la Asia magharibi hususan bara Hindi una umuhimu kwa Iran na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafanya jitihada zote ili kuimarisha amani na utulivu wa kudumu katika eneo hilo na kuhakikisha mataifa ya Kiislamu yanapata haki zao.
Rais wa Iran amesema kuwa, Iran na Pakistan siku zote zimekuwa nchi rafiki, jirani na ndugu na Iran imekuwa ikifanya jitihada kuzuia mivutano na machafuko katika Asia magharibi. Amesema, wakazi wa eneo la Kashmir pia wanapasa kunufaika na maslahi na haki zao za kisheria na kuishi kwa amani na utulivu.
Rais Rouhani ameongeza kuwa suala la Kashmir kamwe haliwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi na masuala kama haya yanapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kidiplomasia.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan ameutaja uhusiano wa Iran na nchi yake kuwa ni wa kirafiki na kidugu na kwamba Pakistan imekumbwa na wasiwasi kutokana na kuuliwa raia wasio na hatia huko Kashmir na kuongezeka mivutano katika eneo hilo. Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni nchi muhimu katika eneo hili na katika Ulimwengu wa Kiislamu, inaweza uwa na nafasi chanya katika kulipatia ufumbuzi suala la Kashmir.
Serikali ya India tarehe 5 mwezi huu ilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura muswada wa kufuta mamlaka maalumu liliyopewa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na nchi hiyo ya kujiendeshea mambo yake.
Hata hivyo wakazi wa eneo hilo wanataka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalosisitiza kufanyika kura ya maoni ya kuaninisha hali ya eneo hilo. Serikali ya India inapinga jambo hilo.