Rouhani: Wananchi wa Iran watasimama kidete mbele ya njama za maajinabi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia njama za maadui ambao wanalenga kutoa pigo kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: "Wananchi wa Iran wamesimama kidete mbele ya njama za maajinabi"
Rais Rouhani ameyasema hayo mapema leo asubuhi katika hafla ya kujadidisha utiifu wa Baraza la Mawaziri kwa malengo matakatifu ya Imam Khomeini MA katika Haram Takatifu ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu kusini mwa Tehran. Huku akimuenzi Hayati Imam Khomeini na Mashahidi Mohammad Ali Rajai na Mohammad Javad Bahonar, Rais Rouhani amesema: "Imepita miaka 40 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hivi sasa Iran imeibuka kama dola lenye nguvu katika eneo nyeti la Mashariki ya Kati kutokana na kusimama imara mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu."
Rais Rouhani amesisitiza kuwa, umoja na kusimama kidete wakuu wote na wananchi wa Iran, ni jambo ambalo limemfanya adui apoteza matumaini. Ameongeza kuwa: "Njama za maadui zitafika ukingoni pale adui atakapopoteza matumaini kabisa kuhusu njama zake za kutaka kutoa pigo dhidi ya Mfumo wa Kiislamu na kwa hivyo lengo kuu la Iran ni kumfanya adui apoteze matumaini."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa,Iran itatumia uwezo wake wote kuwa na uhusiano mzuri na dunia na kuongeza kuwa serikali ya kianagenzi ya Marekani imewasababishia wananchi wa Iran zahma kubwa bali hata wananchi wa eneo hili na Wamarekani pia.
Itakumbukwa kuwa Agosti 30 mwaka 1981 Muhammad Ali Rajai Rais wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu, Hujjatul Islam Walmuslimiin Muhammad Javad Bahonar waliuawa shahidi baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu katika ofisi ya Waziri Mkuu. Jinai hiyo ya kinyama ilitekelezwa na kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO).
Katika kuwaenzi mashahidi hao, baina ya Agosti 24 na 30 huadhimishwa kote Iran kama 'Wiki ya Serikali.