Araqchi: Iran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya JCPOA
(last modified Wed, 04 Sep 2019 07:56:50 GMT )
Sep 04, 2019 07:56 UTC
  • Araqchi: Iran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya JCPOA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema kuwa, Tehran inaamini kwamba hakuna mazungumzo mengine kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini yanaweza kuweko mazungumzo kuhusu utekelezaji kamili wa yaliyoafikiwa ndani ya mapatano hayo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo Jumatano na kumnukuu Abbas Araqchi ambaye yuko mjini Paris Ufaransa tangu siku ya Jumatatu akisema kuwa, ajenda ya mazungumzo yake na serikali ya Ufaransa huko Paris ni namna ya kudhaminiwa matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa kuhusiana na uuzaji mafuta na njia za kuingia Iran mapato ya mauzo hayo.

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itarejea kutekeleza kikamilfu vipengee vya makubaliano ya JCPOA iwapo tu nchi za Ulaya zitaheshimu ahadi zao na Iran ikaweza kuuza mafuta yake na kuingiza nchini fedha zote za  mauzo hayo bila ya vizuizi vyovyote, na hilo ndilo hasa linalojadiliwa katika mapendekezo yaliyotolewa na serikali ya Ufaransa.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA yana baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Naibu huyo wa waziri wa mambo ya nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesisitiza kuwa, nchi za Ulaya zilipaswa kununua mafuta ya Iran au kutoa fidia ya kiwango cha mauzo ya mafuta hayo ambacho ni takriban dola bilioni 15 kwa kipindi cha miezi minne, yaani hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2019.

Amesema, baada ya kupokea dola bilioni 15, wakati huo tena ndipo Jamhuri ya Kisialmu ya Iran itakuwa tayari kufanya mazungumzo na kundi la 4+1 lililobakia kwenye mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo bila ya sababu yoyote.

Tags