Adhama ya Matembezi ya Arubaini kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, Matembezi ya Arubaini ni kitu kisicho na mfano na cha ulimwengu mzima na msingi wa kueneza mafundisho ya Imam Husseini (as) na kuasisi ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana katika hafla ya kuupongeza na kuuenzi ukarimu na moyo wa kupenda wageni walionao watumishi wa Maukibu za Kiiraqi na wahudumu wa Matembezi ya Arubaini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, harakati na mjumuiko adhimu unaoshuhudiwa kila mwaka kwa mnasaba wa Arubaini nchini Iraq na hasa katika msafara wa kutoka Najaf kuelekea Karbala, sasa umechukua sura ya kimataifa. Akaongezea kwa kusema: Mantiki ya Imam Hussein (as) ni mantiki ya kutetea haki na kusimama imara kukabiliana na dhulma, utaghuti, upotofu na uistikbari; na vijana wa dunia ya leo na mataifa yasiyo na chuki, leo hii wana kiu na wanaihitajia mantiki hii; na harakati adhimu ya Matembezi ya Arubaini inaweza kuitambulisha dunia mafundisho na mantiki ya Imam Hussein (as).
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kuhusu umuhimu na ujumbe kwa dunia nzima uliomo katika matembezi adhimu ya Arubaini inabainisha uhakika usioweza kukanushika. Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, kuhudhuria mamilioni ya mazuwari huko Karbala katika maombolezo ya Arubaini ni ishara ya kuamka umma wa Kiislamu katika kukabiliana na njama za maadui za kuufarakanisha umma huo; na ni alama ya kufanikiwa na kupata ushindi hatimaye, mrengo wa harakati ya Imam Hussein dhidi ya mrengo wa ukafiri na uistikbari.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema, matembezi hayo makubwa ni dhihirisho la mchemko wa damu ya Imam Hussein (as) na dhihirisho la ujumbe wa Ashura baada ya kupita 1400; na akafafanua kwa kusema: "Imam Hussein (as) hawahusu Mashia peke yao, bali anazihusu madhehebu zote za Kiislamu zikiwemo za Shia na Suni na anawahusu wanadamu wote; na ndio maana tunashuhudia hata wasio Waislamu pia wanashiriki kwenye Matembezi ya Arubaini."
Katika harakati hiyo kubwa, mchanganyiko wa kiitikadi, kiutamaduni na kihistoria wa mataifa mawili ya Iran na Iraq ni wenye taathira kubwa. Kila mwaka, mamilioni ya mazuwari kutoka Iran huwa wanakirimiwa na kuhudumiwa na wananchi wa Iraq katika matembezi makubwa ya Arubaini; na hii ni ishara ya kuwa kitu kimoja nyoyo za watu wa mataifa mawili hayo ya Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezielezea Iran na Iraq kuwa ni mataifa mawili ambayo, nyoyo na nafsi za watu wao zimeungana pamoja. Ayatullah Khamenei amelifafanua hilo kwa kusema: Maadui wamechukua hatua nyingi za kuzusha mfarakano baina ya mataifa haya mawili, lakini kwa rehma za Mwenyezi Mungu hawakuweza; na baada ya hapa pia hawataweza; kwa sababu suala kuu linaloyaunganisha mataifa mawili ya Iran na Iraq ni imani juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, mapenzi yao kwa Ahlul Bayt (Alayhimu-Salam) na mapenzi makubwa waliyonayo kwa Imam Hussein (as).
Ni wazi kuwa, Wamagharibi wameshindwa kulielewa barabara na kulihakiki tukio hilo lenye adhama ya kipekee la Matembezi ya Arubaini. Kama alivyowahi kueleza hapo kabla pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, kwa muda wa miaka kadhaa, Wamagharibi waliamua kutumia mbinu ya "njama ya kunyamazia kimya" kuhusiana na kuiakisi harakati hiyo adhimu. Lakini hivi sasa wamekuwa hawana budi kuyakubali na kuyazungumzia Matembezi ya Arubaini, ambayo ni hakika yenye taathira, inayotokana na falsafa na ujumbe wa Ashura. Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kuhusu ulazima wa kuongezwa ukwasi wa kimaanawi na kiutamaduni wa Matembezi ya Arubaini linaashiria nukta hiyo na kubainisha pia umuhimu wa maadhimisho yenye haiba na adhama ya kipekee ya matembezi hayo kwa mtazamo wa ulimwengu mzima.
Ayatullah Khamenei ametoa mwito pia kwa wanafikra na wanautamaduni kuandaa ratiba maalumu kwa ajili ya harakati hiyo adhimu; na akalibainisha hilo kwa kusema: Matembezi ya Arubaini yanaweza kuwa msingi wa kufikia ghaya na lengo kuu la umma wa Kiislamu, yaani "Kujenga Ustaarabu Adhimu na Mpya wa Kiislamu"; na kwa sababu hiyo inapasa kuzidisha mafungamano imara yaliyopo baina ya Waislamu wakiwemo Mashia na Masuni pamoja na mataifa na kaumu mbali mbali katika matembezi haya.
Hapana shaka yoyote kuwa, harakati isiyo na mfano ya Matembezi ya Arubaini ni yenye thamani za kimaanawi na inatokota joto la imani ya mwamko na vuguvugu la kihistoria la Ashura; na kwa hakika ghairi ya hayo, hakuna kitu kingine chochote chenye uwezo kutoa msukumo wa kufanyika harakati kama hiyo. Na ndio maana Matembezi ya Arubaini yanazidi kuchukua sura ya kimataifa na ya ulimwengu mzima, siku baada ya siku.
Ni kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kusema: Ikiwa uwezo na fursa zisizohesabika yalizonazo mataifa ya Kiislamu katika Magharibi ya Asia na Kaskazini mwa Afrika zitaunganishwa pamoja na zikafanyiwa kazi kivitendo, hapo ndipo walimwengu watadhihirikiwa na maana halisi ya izza inayotokana na Allah na ustaarabu adhimu wa Kiislamu.../