Zarif: Iran haitoanzisha vita vya aina yoyote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha kwamba Iran haitoanzisha vita vyovyote, amesema kuwa, iwapo Tehran itashambuliwa, basi itajitetea kwa uwezo wake wote.
Mohammad Javad Zarif ambaye yupo mjini New York kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya CNN na kuongeza kuwa, kwa mara kadhaa Iran imeionya Marekani kuwa iwapo itaanzisha vita, basi hatima ya vita hivyo haitokuwa mikononi mwa Washington.
Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Benki Kuu ya taifa hili na kusema kuwa, vikwazo ni zaidi ya vita kwa kuwa vikwazo vinawalenga raia wa kawaida.
Mohammad Javad Zarif amesisitia ulazima wa serikali ya Marekani kuhitimisha vikwazo dhidi ya Iran na kuesema kuwa, serikali ya Rais Donald Trump inatakiwa kwanza ifute vikwazo vyake vya daima dhidi ya Iran katika Bunge la Kongresi la nchi hiyo.
Kadhalika amekadhibisha madai ya kuhusika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika shambulizi dhidi ya taasisi za mafuta za ARAMCO nchini Saudia na kusema kuwa, silaha za Wayemen zimeshinda silaha za kijeshi za kisasa zaidi na nzito zaidi za Marekani ilizonazo Saudia.