Iran: Nchi za eneo zijue kwamba usalama si kitu cha kununua
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu inataka usalama wa Ghuba ya Uajemi uletwe na nchi zenyewe za eneo na akasisitiza kuwa: Nchi za eneo zielewe kwamba usalama si kitu cha kununua.
Sayyid Abbas Mousavi ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi na akaongeza kuwa: Iran inataka amani, usalama, uthabiti na maendeleo katika eneo, na kwamba hayo yatapatikana kwa ushirikiano wa kieneo, si kwa kununua kutoka nje.
Akijibu suali kuhusu madai ya Saudi Arabia kwamba Iran inatuma silaha Yemen, Mousavi amesema: Yemen imewekewa mzingiro mkali kabisa, kiasi kwamba haiwezekani kuifikishia nchi hiyo hata misaada ya kibinadamu; kwa hivyo uzushaji madai hayo hauna msingi wala mashiko yoyote.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, njia pekee kwa Saudia kujitoa kwenye mgogoro wa Yemen ni kukubali usitishaji vita na kuondoa mzingiro ilioiwekea Yemen; na akaeleza matumaini aliyonayo kwamba, baada ya usitishaji vita itaweza kupatikana njia pia ya kupeleka misaada ya kibinadamu nchini Yemen.
Kuhusu uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Afghanistan, Mousavi amesema, Iran ni muungaji mkono wa Afghanistan yenye amani na uthabiti na inaunga mkono pia utaratibu wa uchaguzi unaofuatwa na serikali na wananchi wa nchi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia pia madai ya gazeti la The Gurdian la Uingereza kwamba nchi za Ulaya zimetishia kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA endapo Iran itaendelea kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano hayo kwa kusema: "Iran inatekeleza hatua za kujifidia kwa kutumia kifungu cha 26 na 36 vya JCPOA, kwa hivyo jibu la Ulaya kuhusiana na hatua za Iran halikubaliki.../