Salami: Stratijia ya muqawama imepelekea adui akose irada
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema stratijia ya muqawama au mapambano ya Kiislamu imepelekea adui adorore na akose irada. Ameongeza kuwa, hivi sasa maadui wameanza kudidimia kwa namna ambayo hawawezi kupata nguvu tena na hifadhi zao za kistratijia zinaelekea kumalizika.
Meja Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC aliyasema hayo jana Jumatatu mjini Tehran katika ufunguzi wa Kongamano la 23 la Kitaifa la Makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika hotuba yake alisisitiza kuwa, itibari na nguvu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu inazidi kuimarika. Ameongeza kuwa, leo si tu kuwa adui anarudi nyuma kutoka maeneo ya kijiografia aliyokuwa anayadhibiti huko nyuma bali pia vikwazo vya kiuchumi alivyoweka dhidi ya taifa la Iran navyo pia havina athari.
Meja Jenerali Salami amesisitiza kuwa, leo Iran ina uwezo wa kumshambulia adui kwa uwezo mkubwa na katika eneo kubwa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Iran ina uwezo wa kuuangamiza utawala wa Kizayuni wa Israel na inaweza kuuondoa utawala huo katika jiografia ya dunia.
Akizungumza katika kikao hicho, Hujjatul Ibrahim Raisi, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran amesisitiza kuwa, kwa kutungua drone vamizi ya Marekani, IRGC imeweza kuwaonyesha walimwengu kuwa nguvu za Marekani ni bandia. Amesema maadui hawawezi kustahamili uwezo mkubwa wa kambi ya muqawama.