Zarif: Kipaumbele cha Iran ni uhusiano mwema na nchi jirani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kustawishwa uhusiano na nchi jirani ni kipaumbele muhimu katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo leo alipohutubu katika Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, na kuongeza kuwa: "Uhusiano wa Iran na Afghanistan, Pakistan, Russia, Uturuki na Qatar haujawahi kuwa mzuri kama ilivyo hivi sasa."
Zarif ameendelea kubaini kuwa, ili kupunguza hujuma za kigaidi kuna haja ya kutumiwa uwezo wa viongozi wa eneo, viongozi wa kidini na pia wabunge.
Akiashiria hali ya mambo nchini Afghanistan, Zarif amesema Iran inataka kuona amani katika nchi hiyo na hilo litawezekana tu kwa kushirikishwa pande zote husika nchini humo.
Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema raia wawili wa Iran ambao walikuwa wanashikiliwa katika magereza ya nje ya nchi kwa tuhuma zisizo na msingi wameachiliwa huru.
Reza Dehbashi mwanachuo wa Iran katika Chuo Kikuu cha Queensland Australia alikamatwa Mei 13 kwa tuhuma zisizo na msingi za kujaribu kutoa msaada kwa mfumo wa kujilinda wa Iran. Hatimaye kufuatia jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameachiliwa huru na amerejea mjini Tehran.
Naye Negar Ghodskani, mwanamke Muirani mwenye umri wa miaka 40 ambaye alikamatwa Australia mwaka 2017 kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, na kisha kuhamishiwa Marekani Julai 2019, ameachiliwa huru kufuatia amri ya mahakama katika jimbo la Minnesota.