Iran: Dhima ya kushambuliwa meli yetu ya mafuta iko kwa wafanya chokochoko
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza hisia zake baada ya kushambuliwa meli ya mafuta ya Iran katika Bahari Nyekundu na kusema kuwa, dhima yote ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira uliosababishwa na kushambuliwa meli hiyo iko juu ya wanaofanya chokochoko kwenye eneo hili.
Sayyid Abbas Mousavi ameongeza kuwa, uchunguzi uliofanywa na Shirika la Taifa la Mafuta la Iran unaonesha kuwa meli moja ya mafuta ya Iran leo Ijumaa asubuhi imeshambuliwa mara mbili kwenye Bahari Nyekundu katika mashambulizi yaliyopishana kwa takriban nusu saa.
Amesema mafuta yaliyokuwa yanamwagika kwenye meli hiyo yamezuiwa na Alhamdulillah hakuna mfanyakazi yeyote wa meli hiyo aliyepata madhara.
Amesema, miezi kadhaa iliyopita pia, kulitokea vitendo vya uharibifu dhidi ya meli za mafuta za Iran katika Bahari Nyekundu na uchunguzi unaendelea kufanywa ili kugundua ni akina nani waliohusika na chokochoko hizo.
Mashirika mbalimbali ya habari nayo yameripoti kuwa , mafuta yaliyokuwa yanavuja kwenye meli hiyo ya mafuta ya Iran iitwayo SABITI yameweza kudhibitiwa.
Shirika la habari la IRNA ni miongoni mwa mashirika yaliyoripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, hakuna moto wowote uliotokea kwenye meli hiyo na meli iko katika hali ya usalama na utulivu kikamilifu.
Baadhi ya habari zinasema kuwa meli hiyo imeshambuliwa kigaidi. Tukio hilo limetokea katika umbali wa meli 60 kutoka bandari ya Jeddah ya Saudi Arabia.