Ayatullah Khamenei: Tunafuata nyayo za Sayyidu Shuhadaa, hatutasalimu amri mbele ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56599-ayatullah_khamenei_tunafuata_nyayo_za_sayyidu_shuhadaa_hatutasalimu_amri_mbele_ya_marekani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kwa mujibu wa falsafa ya harakati ya Bwana wa Mashahidi (Imam Hussein bin Ali (as)), taifa la Iran linakutambua kupambana na kambi ya ukafiri, uzayuni na Marekani kuwa ni wajibu wake, na kutosalimu amri kwa Iran mbele ya Marekani kunafanyika kwa msingi huo.
(last modified 2026-09-03T12:21:49+00:00 )
Oct 13, 2019 08:55 UTC
  • Ayatullah Khamenei: Tunafuata nyayo za Sayyidu Shuhadaa, hatutasalimu amri mbele ya Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kwa mujibu wa falsafa ya harakati ya Bwana wa Mashahidi (Imam Hussein bin Ali (as)), taifa la Iran linakutambua kupambana na kambi ya ukafiri, uzayuni na Marekani kuwa ni wajibu wake, na kutosalimu amri kwa Iran mbele ya Marekani kunafanyika kwa msingi huo.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo asubuhi ya leo katika hadhara ya wanafunzi wa Chuo cha Jeshi cha Imam Hussein (as) ambako amekumbusha izza na heshima ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) ndani na nje ya Iran na kusema: Wamarekani pia wamezidisha heshima ya jeshi la Sepah kwa sura yao ya kihasama na iliyojikunja.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kujizatiti katika pande zote na kusisitiza kuwa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali (as) ni kieleelzo cha nguvu na uwezo halisi na kuongeza kuwa: Mkusanyiko mkubwa wa mamilioni ya mazuwari na wafanyaziara wanaoelekea Karbala wanadhihirisha tena nguvu ya Uislamu na kambi ya mapambano ya Kiislamu.

Amesema kuwa, matembezi adhimu ya Waislamu kutoka nchi mbalimbali, makundi tofauti ya Kiislamu na hata kutoka baadhi ya dini nyingine katika Arubaini ya Imam Hussein ni sauti madhubuti na chombo cha habari kisicho na kifani katika dunia tata ya propaganda ya mwanadamu wa leo. Ameongeza kuwa: Kaulimbiu yenye maana pana ya "Hussein Yajmauna" yaani 'Hussein anatukutanisha pamoja sote' ni uhakika halisi, kwa sababu Imam Hussein (as) ndiye mwanzilishi wa mkusanyiko huo usio na kifani, na washiriki wote wanaelekea katika chemchemi ya masuala ya kiroho na kujikomboa.

Ayatullah Ali Khamenei akikagua jeshi la Sepah

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, hii leo kambi ya ukafiri, uzayuni na Marekani inaamilia na mataifa mbalimbali kwa dhulma na ukandamizaji kupitia njia ya kunyonya damu zao, kuanzisha vita na kufanya maafa mengine. Amesisitiza kuwa, Imam Hussein (as) alikutaja kutekeleza wajibu wa kupambana na dhulma na madhalimu kuwa ndiyo sababu ya harakati na mapambano yake na kwa msingi huo huo Jamhuri ya Kiislamu inatambua kwamba, ni wajibu wake kutekeleza wadhifa huo na itautekeleza katika hali zote. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Vijana wanapaswa kuelewa kwamba, fikra na akili zao ndio mlengwa wa kwanza wa mashambulizi ya adui; hivyo wanapaswa kusimama kidete kwa imani na nguvu zao zote mbele ya njama za maadui.