Matamshi ya Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Pakistan
Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazungumzo yake na Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan na ujumbe alioandamana nao ziarani hapa Tehran, ameutaja uhusiano wa Iran na Pakistan kuwa ni mkubwa na wa kidugu.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jana alasiri, Kiongozi Muadhamu aliweka wazi daghadagha zinazoikabili serikali ya Pakistan kuhusu urejeshaji amani na usalama na kulitaja eneo la Asia Magharibi kuwa nyeti sana na hatari. Aidha amesisitiza kuwa, pande zote zinapasa kuchukua hatua za lazima ili kuzuia matukio mbalimbali yasiyotakikana na kueleza kusikitishwa kwake na nafasi haribifu ya baadhi ya nchi katika eneo katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria na kuibua vita na umwagaji damu nchini Yemen.
Tukitupia jicho matukio ya miaka kadhaa ya karibuni katika eneo na jinai zilizofanywa na kundi la Daesh na magaidi wengine wanaoungwa mkono na Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni, na pia vita vya kidhalimu dhidi ya Yemen tunaona kuwa, ukosefu wa amani na vita vya kila uchao havijakuwa na natija yoyote ghairi ya kuyasababishia mataifa ya eneo hili umwagaji damu, kuuawa wanawake na watoto, kuwafanya raia kuwa wakimbizi na kusababisha hasara na maafa chungu nzima. Hata hivyo kumalizika machafuko haya tajwa kunategemea irada ya pande mbalimbali zilizoibua hali hii ya mivutano na vita vya niaba sambamba na kuzusha migogoro kutokana na uingiliaji wa nchi ajinabi.
Iran na Pakistan zinaaminikuwa masuala ya eneo yanapasa kupatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo kati ya nchi mbalimbali. Imran Khan amesisitiza juu ya nukta hii kwamba, moja ya malengo ya safari yake hapa Tehran ni kufanya mazungumzo ili kupunguza hali ya mvutano katika eneo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuhusu nia njema ya pande mbili na kufanyika jitihada ili kulinda amani na uthabiti katika eneo kwa kuzishirikisha nchi zote jirani; na katika uwanja huo, imewasilisha mpango kuhusu amani ya eneo la Ghuba ya Uajemi na vile vile kuhitimisha vita huko Yemen. Mpango huo wenye marhala nne unajumuisha usitishaji vita, kutumwa misaada ya kibinadamu, kufanyika mazungumzo kati ya makundi ya Wayemeni na kuunda serikali shirikishi nchini kwa kuyajumuisha makundi ya mirengo mbalimbali ya nchi hiyo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa pia ipo tayari kushiriki katika mazungumzo yanayolenga kufanikisha utekelezaji wa mpango huo wa amani kwa kuwashirikisha washikadau wote.
Matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Pakistan yamebainisha wazi jambo hilo. Ayatullah Khamenei aidha amekumbushia nukta hii kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu huko nyuma imewasilisha mpango huo wa vipengee vinne kwa ajili ya kuhitimisha vita huko Yemen na kuongeza kuwa: Iwapo vita hivyo vitahitimishwa kwa njia sahihi, basi kunaweza kushuhudiwa taathira chanya katika eneo.
Kiongozi Muadhamu pia amebainisha kuwa: Sisi hatuna nia ya kuwa na uadui na nchi hizo hata hivyo nchi hizo zinaendeshwa kwa matakwa ya Marekani, na zinachukua hatua dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mujibu wa matakwa ya Marekani. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuanzisha vita vyovyote vile lakini yoyote atakayeanzisha vita dhidi ya Iran bila shaka atajutia jambo hilo.
Ni dhahir shahir kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimejengeka katika msingi wa kujiweka mbali na mivutano na mapigano ya kijeshi. Iran inaamini kuwa ufumbuzi wa matatizo ya eneo unahitajia mazungumzo ya nia njema, usalana na kuimarishwa uhusiano wa kieneo. Ni kwa msingi huo ndio maana Rais Hassan Rouhani wa Iran pia akagusia katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na na Waziri Mkuu wa Pakistan juu ya suala la usalama wa eneo na kusisitiza kuwa: Tehran na Islamabad zinaamini kuwa, ufunguo wa utatuzi wa masuala ya eneo ni kuhitimishwa vita huko Yemen haraka iwezekanavyo. Kuhusu suala hilo, naye Waziri Mkuu wa Pakistan amesisitiza kuwa, usitishaji vita huko Yemen unaweza kuwa mwanzo wa kutekelezwa mchakato wa amani, kuondoa hali ya mivutano katika eneo na kufanyika mazungumzo ya pande mbili na kadhaa katika uwanja huo.