Abbas Mousavi: Vikwazo vya kukaririwa vya Marekani havitaifikisha popote Washington
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Tehran na kusema kuwa, vikwazo vya kukaririwa vya Washington havitalifikisha katika malengo yake taifa hilo la Magharibi.
Sayyid Abbas Mousavi amesema kuwa, hatua kama hizi za Marekani ni ishara ya udhaifu na kushindwa kidiplomasia nchi hiyo.
Wizara ya Fedha ya Marekani siku ya Jumatano ilitoa taarifa na kutangaza vikwazo dhidi ya taasisi 21 na watu wanne wanaohusiana na Iran na makundi ya muqawama. Marekani imesema vikwazo hivyo vitatekelezwa kwa ushirikiano na waitifaki wake wa kieneo ambao ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Imarati na Saudia.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, inasikitisha kuwa, chombo cha kidiplomasia cha Marekani hakina uwezo wa kufanya ubunifu na kuwa na mikakati na mbinu za kidiplomasia zenye kukubalika kiakili na badala yake Washington inakimbilia kwenye utumiaji mabavu na ugaidi na kiuchumi.
Sayyid Abbas Mousavi aidha amebainisha kwamba, ubeberu na utumiaji mabavu wa serikali ya Marekani katika mahusiano yake na mataifa mengine ya dunia umegeuka na kuwa tatizo la kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Marekani inapaswa kuachana na ndoto zake za alinacha na badala yake itekeleze majukumu yake iliyojifunga nayo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.