Iran yaanza kuweka gesi katika mashinepewa za kizazi cha kisasa
Oparesheni ya kuweka gesi ya uranium hexafluoride (UF6) katika injini za mashinepewa (centrifuge) za kisasa aina ya IR 6 imeanza katika Kituo cha Kurutubisha Urani cha Natanz katika sherehe iliyohudhuriwa na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi.
Katika sherehe hiyo iliyofanyika Jumatatu katika katika kituo hicho kilichoko kati mwa Iran, pia kulizinduliwa kizazi kipya cha mashinepewa hizo za IR 6. Akizungumza katika hafla hiyo, Ali Akbar Salehi amesema: "Mashinepewa hizi zinaweza kurutubisha urani mara 10 zaidi ya mashinepewa za kizazi cha kwanza."
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebaini kuwa, uwezo wa urutubishaji urani wa Iran sasa umefika SWU 8,660 na kuongeza kuwa: "Uzalishaji urani ambao ulikuwa ukifanyika Iran kabla ya kuchukuliwa Hatua ya Tatu ya Kupunguza Uwajibikaji katika JCPOA, ulikuwa ni gramu 450 kwa siku na sasa kiwango hicho kimefika zaidi ya garmu 5000 kwa siku.
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kwa muda mrefu sasa urutubishaji urani Iran umekuwa ukifanyika kwa kutumia mashinepewa za kizazi cha kwanza za IR1 na kuongeza kuwa: "Kile ambacho kimefanyika leo kilipaswa kufanyika miaka minne iliyopita lakini changamoto za kisiasa ambazo zimeibuliwa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran zimepelekea wakuu wa Iran wachukue uamuzi wa sasa."
Salehi ameongeza kuwa wasomi wa nyuklia wa Iran wanaendelea na kazi zao za ustawi katika uga huo.
Ikumbukwe kuwa mnano Mei 8 2018, Marekani ilichukua uamuzi wa upande mmoja na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na madola makubwa duniani ya kundi la 5+1 yaliyofikiwa mwaka 2015.
Kufuatia uhasama huo wa Marekani, Iran ilichukua hatua ya kistratijia ya kusubiri kwa muda wa mwaka mmoja ili kuona iwapo nchi zilizosalia katika JCPOA zingekidhi matarajio yake. Baada ya nchi hizo kutochukua hatua za maana za kukabiliana na kujiondoa Marekani katika JCPOA, Iran hadi sasa imechukua hatua 3 za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo.