Iran yaanza urutubishaji urani katika kiwango cha asilimia 60
Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema: "Uzalishaji urani katika kiwango cha asilimia 60 umeanza katika Kituo cha Nyuklia cha Fordo."
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, IRNA, Mohammad Eslami Rais wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alitoa tamko hilo Jumanne pembizoni mwa Maonyesho ya 20 ya Mazingira ya Iran wakati akijibu swali kuhusu jawabu la Iran kwa azimio la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Eslami ameongeza kuwa, "Mashinikizo na maazimio ya kisiasa hayabadilishi chochote. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu kali kwa azimio lolote dhidi yake."
Eslami amesema: "Hivi sasa, zaidi ya mapipa milioni saba ya mafuta yameokolewa tangu operesheni ya kituo cha kuzalisha umeme cha Bushehr ilipoanza, na kwa kuzingatia msisitizo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya matumizi ya nishati safi, sheria ya kulenga maendeleo ya nyuklia na kustawisha mitambo ya kuzalisha umeme wa nyuklia iko kwenye ajenda ili kuwa na ongezeko la utumiaji wa nishati ya nyuklia hadi 20%.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa: Katika Shirika la Nishati ya Atomiki, hatua zinapaswa kuchukuliwa katika sekta mbili za uzalishaji wa umeme kutokana na teknolojia ya nyuklia na ujenzi wa vifaa vya kupunguza uchafuzi wa mazingira."
Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki iliidhinisha azimio dhidi ya shughuli za amani za nyuklia za Iran katika mkutano wake wa robo mwaka Alhamisi iliyopita chini ya shinikizo kubwa la kisiasa kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
Hili ni azimio la tatu la Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki dhidi ya Iran baada ya kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA .