Iran: Ripoti ya IAEA imetolewa kwa mujibu wa matashi ya kisiasa
Iran imetoa wito kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuakisi hali halisi kuhusu mpango wa amani wa nishati ya nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu na kujiepusha na matashi ya kisiasa kwenye ufuatiliaji wake wa shughuli za nyuklia za nchi hii.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi alitoa mwito huo wakati wa mazungumzo yake ya simu na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi jana Jumamosi.
Katika mazungumzo hayo ya simu, maafisa hao wamejadili, miongoni mwa mambo mengine, ripoti mpya iliyochapishwa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, "Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) haupaswi kutoa maoni kwa kuzingatia mitazamo ya kisiasa."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, matarajio ya Iran kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ni kwamba afanye kazi ndani ya mipaka ya mamlaka na majukumu yake na kwa mujibu wa sheria na kanuni za shirika hilo.
Araghchi amebainisha kuwa, kutoa maoni kwa msingi wa uvumi na tetesi za kisiasa hakuko ndani ya mamlaka ya Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, na wala hakusaidii kutatua lolote, na badala yake kunachochea anga na kuzuia mangiliano yenye kujenga.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, mpango wa nyuklia wa Iran umethibitishwa mara nyingi kuwa unatekelezwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Mazungumzo ya Araghchi na Grossi yamekuja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) kutoa taarifa ya pamoja, iliyokosoa vikali ripoti hiyo ya IAEA iliyoishutumu Jamhuri ya Kiislamu kwa kile ambacho IAEA imedai, eti Tehran kuzidisha urutubishaji wa urani kwa kiwango cha juu sana. Taarifa hiyo imesema ripoti hiyo imetolewa kwa kutegemea nyaraka ghushi zinazotolewa na utawala wa Israel.