Russia yaunga mkono hatua ya nne ya Iran kuhusu JCPOA
(last modified Tue, 05 Nov 2019 14:31:22 GMT )
Nov 05, 2019 14:31 UTC
  • Sergei Ryabkov
    Sergei Ryabkov

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametangaza kuwa hatua ya nne iliyochukuliwa na Iran kwa ajili ya kupunguza utekelezaji wa majukumu yake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni jambo la kimantiki.

Sergei Ryabkov amesema Moscow haikushangazwa na uamuzi iliochukuliwa na Iran wa kupunguza utekelezaji wake wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, Marekani ndiyo ya kulaumiwa kutokana na hali ya sasa ya makubaliano hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, kuzinduliwa kwa mashinepewa mpya katika kituo cha kuruutubisha madini ya nyuklia cha Fordow hakuna maana ya kuvunjwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Ryabkov amesisitiza kuwa, mpango wa pamoja wa Iran na Russia wa kukibadilisha kituo cha kurutubisha urani cha Fordow na kuwa kituo cha masuala ya utafiti na ustawi bado uko mezani.

Mapema leo Rais Hassan Rouhani ametangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatekeleza hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuanzia kesho.

Rais Hassan Rouhani

Rais Rouhani amesema kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, iliamuliwa kuwa, mashinepewa 1044 ziendelee kuzunguka katika kituo cha Fordow bila ya kuwekwa gesi katika zana hizo, lakini sasa tangu kesho Jumatano tutaanza kuweka gesi katika mashinepewa za Fordow.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa pande zote zinapaswa kuelewa wkamba Iran hauwezi kuwa mtekelezaji pekee wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi amesema kuwa, "mashinepewa hizi za kizazi kipya zinaweza kurutubisha urani mara 10 zaidi ya mashinepewa za kizazi cha kwanza."

Hadi sasa Iran imechukua hatua 3 za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo ya nyuklia baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo na kushindwa nchi za Ulaya kutekelezaji majukumu yao.

Tags