Mousavi: Makubaliano ya Riyadh hayatosaidia kutatua matatizo ya Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi, amesema kuhusu makubaliano ya Riyadh yaliyofikiwa kati ya baadhi ya makundi ya kusini mwa Yemen na Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu, kwamba kusainiwa hati kama hiyo ya makubaliano hakutasaidia chochote katika kutatua matatizo ya Yemen.
Jana Jumanne, vikosi vitiifu kwa Mansur Hadi, rais wa Yemen aliyejiuzulu, vyenye mfungamano na Saudi Arabia vilisaini hati ya makubaliano na baraza la mpito la kusini lenye mfungamano na Imarati, katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Mousavi ameongeza kuwa, makubaliano ya Riyadh yanalenga kuuzatiti uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu wa Saudia na waitifaki wake huko kusini mwa Yemen kwa njia ya moja kwa moja au kupitia vikosi vya niaba.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa: Wananchi werevu na walio macho wa Yemen, ambao daima wamepambana na wavamizi, hawataruhusu eneo la kusini la ardhi ya nchi yao lidhibitiwe na maadui na wasiowatakia mema, na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya maajinabi.
Vile vile ameiasa Saudi Arabia kwamba: Kama kweli, kama inavyodai, ina nia ya dhati ya kutatua kadhia ya Yemen, basi badala ya kuyapitishia maamuzi makundi yasiyo na mamlaka yoyote, itoe jibu chanya kwa kuitikia mwito na pendekezo lililotolewa na Mahdi Mushat, mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen la kusimamishwa mashambulio baina ya nchi mbili.
Sayyid Abbas Mousavi amesisitizia kulindwa umoja wa ardhi yote ya Yemen na kukumbusha kuwa: Kama ilivyosisitiza mara kadhaa, Iran inaitakidi kwamba, hatua ya kwanza ya kutatua mgogoro wa Yemen ni kusitishwa vita na umwagaji damu na kuondolewa mzingiro wa kidhalimu iliowekewa nchi hiyo; na hatua inayofuata ni kufanyika mazungumzo baina ya Wayemeni wenyewe ili kufikia mwafaka juu ya mustakabali wa kisiasa wa nchi yao.../